ADUI YETU

Regani,bosi wa kampuni ya teknolojia ambayo inayomilikiwa na wamarekani, hakua mtu wa kauli mbili katika uendeshaji wake wa kampuni.Hakuzoeana na wafanyakazi wenzake,na hiyo kufanya wengi wao kutomfahamu vyema na pengine kumwogopa kiasi.

Mwishoni mwa kila mwaka kampuni hii ya teknolojia ilituma wajumbe kutoka Marekani,kuja kusheherekea kumaliza mwaka pamoja na kutoa tuzo kwa mfanyakazi bora.Kwa miaka miwili mfululizo tuzo hii imekua ikichukuliwa na Regani,na wafanyakazi wote waliamini kuwa ni ngumu sana kwa mfanyakazi mwingine kupata tuzo hiyo.

Wafanyakazi wa kampuni hii, walioajiriwa na makao makuu waliwajibika moja kwa moja katika ofisi kuu ya Marekani,isipokua tu kwa wale waliokua vibarua.Hivyo utendaji wa mfanyakazi yeyote ungeweza kupimwa pasina mashaka.Wafanyakazi wengi walimchukia sana Regani na kuamini kuwa alikua ‘akiwachongea’kwa mabosi wao na hivyo kupelekea wao kupunguziwa mishahara na kutokupata tuzo.

Kipindi hiki mambo yalibadilika sana,tuzo ya mfanyakazi bora ilikwenda kwa Gray,kijana mpole na mstaarabu sana.Kijana huyu ndo kwanza alimaliza mwaka tangu afanye kazi na kampuni hii.Hili halikuwashtua tu wafanyakazi wengine bali hata Regan, ni kama hakulielewa hili tangu awali.

Baada ya maadhimisho ya sherehe za mwisho wa mwaka na sherehe ya kutuzwa kupita,Kila kitu kilianza kubadilika kwenye kampuni.Regani alikua akijiuliza ni kwa jinsi gani yule kijana mgeni ameweza kutuzwa tuzo ile na ni kitu gani alichofanya tofauti na yeye.Wafanyakazi nao walipigwa na butwaa na walianza kufikiri kuwa yule kijana ndo aliyekuwa anawaharibia mambo.

Adui yetu ni nani?

Pengine ni swali ambalo limekua miongoni mwa watu wengi pale ambapo wameshindwa kufanikiwa,kufikia ndoto zao au malengo yao.Kila mtu humtafuta mchawi wa mafanikio yake,na kwa namna yeyote ile kila mtu lazima apate mtu wa kumbebesha lawama za kufeli kwake.

Kila mtu hutafuta adui yeyote ili kuaminisha umma kwamba sio yeye aliyefeli,bali kuna mtu nyuma yake au hata mazingira.Mara nyingi tunatumia nguvu kubwa kupambana na adui wa nje kabla ya kumshinda adui aliye ndani yetu.Choyo,husuda,wivu,chuki,ubinafsi uliokithiri ndio maadui wakubwa ambao wametutafuna ndani kwa kiasi ambacho hatuwezi kuona na tukaamua kutafuta maadui wa nje wa kuficha yaliyo ndani yetu.

Ni dhahiri kuwa, itakua ngumu sana kumshinda adui wa nje kama tumejishindwa wenyewe.Adui yetu anakula na sisi,analala na sisi na amekua mshauri wetu pale tunapotafuta mchawi wa mafanikio yetu.Adui huyu amestarehe kabisa kwani hakuna anayeshughulika nae,tumemliwaza na kumsahaulisha kuwa anatakiwa kutokua ndani yetu.Adui huyu amekua akifurahi sana pale tunapokua tukipambana na maadui wa nje,akijipa moyo kuwa yeye tayari amesahaulika.Tamaa iliyokithiri na wivu wa ndani umeongeza chachu ya kuwaona wanaofanikiwa kama maadui zetu haswa.Tumekua tukitengeneza uadui na kila wenye mafanikio zaidi yetu pasipo sababu muhimu.Tumewaona hawafai kuwa kwenye nafasi walizopo na sisi ndio tunafaa zaidi.Chuki binafsi imekula nafsi zetu,kuwachukia wenzetu pasina sababu kumekua adui yetu anayetumaliza hasa.

Nimejifunza jambo moja katika maisha,kila unapofikiri umemmaliza adui mmoja wa nje huwa anaibuka mwingine mwenye nguvu sawa na yule.Ni dhahiri kuwa baada ya wafanyakazi kumchoka Regani kama adui yao tayari walipata adui yao mwingine,na haitaishia hapo kila atakaye pokea tuzo hii au kuwa na cheo katika kampuni hii ataendelea kuwa Adui yao tu.

Kabla hatujapambana na adui wa nje tuhakikishe hayupo adui ndani yetu,maana ni vigumu kuona mtu kafanya vizuri(kafanikiwa) na kumpongeza ikiwa una chuki,ubinafsi na wivu.Tujiweze kwanza sisi binafsi kabla ya kujifunza kuwaweza wengine.

ADUI YETU YUPO NDANI YETU

Comments (7)

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 22,653 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: