BARUA YA WAZI KWAKO MPENZI

 

HUJAMBO!

Barua ya wazi kwako mpenzi. Sijakusomesha lakini nahitaji uisome barua yangu ya wazi kwa usikivu na ujue mapenzi niliyo nayo kwako ni ya kudumu. Niazime macho na akili yako walau dakika chache.

Naandika barua hii ikiwa ni mwisho wa mwaka mmoja kwenye Kalenda na mwanzo wa mwaka mwingine mpya. Mwaka ambao ulikuwa tasa kwa maana kwamba haugawanyiki  kwa mbili. Mwaka ambao ulibeba furaha na huzuni za watu, kupata na kukosa pia, zote zilikuwa sifa za mwaka huu.

Mpenzi, Nakuandikia barua hii mwishoni mwa mwaka ila usijiulize kwanini. Sababu zinaweza kuwa nyingi kuliko wingi wa maneno yaliyoko kwenye waraka huu.

Naweza kujiita Mchelewaji wa taifa maana nimekuwa nachelewa kwenye 80% ya mambo yote ninayoyafanya. Hata Kitambulisho cha Taifa cha Tanzania nilipata mwishoni kabisa pale www.nida.go.tz . Na hii ni baada ya hamasa kubwa toka kwa Mhe. Jiwe. Ndio maana nimechelewa kuwasilisha barua hii kwako japo kuchelewa kwake ndiko kumeizidishia umuhimu wake.

Mpenzi, kama unijuavyo mimi sio mwongeaji sana ila naandika sana. Hivyo nashukuru hatukuweza kuonana mwaka 2019 maana kiukweli ningeshindwa kutanabaisha yale yaliyoujaza moyo wangu pomoni. Kutokuonana nawe kumenipa fursa adhimu ya kuweka fikra zangu katika maandishi. Fursa ambayo naona ni njia nzuri yenye mtiririko nyoofu wa mawazo.

Kwenye barua hii ya wazi siwezi kung’ata midomo au kumung’unya maneno hivyo naamini mizizi ya ukweli utaiona, na hata matawi yake utayaona. Kwa lugha rahisi acha “nikuchane mwanangu”

Mpenzi, Waswahili husema “muda ni pesa” kwahiyo acha niende kwenye mada kamili au nyama ya barua hii, barua ya wazi kwako mpenzi.

Nimesikia wengi sana wakilalamika na pengine kumshirikisha Mungu ili waweze kukutana na wewe. Maombi yao nimekuwa nikikumbana nayo kwenye mitandao ya kijamii na kwenye maongezi ya kawaida. Lakini cha ajabu kila mwisho wa mwaka walio wengi huonyesha kutoridhika na kile walichokivuna. Sina hakika kama huwa unaanza nao mwaka na kisha kuwaacha njiani. Kama kweli huwa unaanza nao mwaka na kuwapotea njiani, basi mpenzi wewe nitakuita msaliti. Tena msaliti uliyekubuhu.

Mpenzi, mimi binafsi nimekuwa nikihaha mchana kutwa, kuandika makala, kuandika tweet, hadithi fupi fupi na shughuli nyingine nyingi na za muhimu nje ya mitandao ili siku moja kama ikitokea ukavutiwa na hadithi, riwaya,  tweet au kazi mojawapo ninayoifanya, basi tuwasiliane au uje kwangu tuongee kinagaubagha huku tukiwa kama ndugu baada ya kumaliza tofauti zetu zilizopelekea sisi kutoona kwa miaka yote. Tofauti na matarajio yangu, wewe umekuwa ukinikazia, ukiuchuna, ukila gundi… kiufupi umekuwa ukinitenga mpenzi wangu. Umekuwa ukinibagaza. Umekuwa ukijimwambafai kupita maelezo.

Mpenzi, marafiki na ndugu zangu unawajua. Wapo ambao umeishi nao kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Kwanini sio mimi? Kwanini mimi ninayehangaika kutwa-kucha hutaki kufika kwangu walau uishi miaka kadhaa?

Ni marafiki haohao unaoishi nao ndio wamekuwa wakinikatisha tamaa kwa kunitolea mifano isiyofaa. Mfano: Marafiki zangu wa Twitter wamekuwa wakiniambia kwamba Yule bwana aliyeandika kitabu cha “How to be rich” alikopa fedha benki ili akichapishe kitabu chake hicho. Lakini unaishi nao. Huoni kwamba hii ni roho mbaya?

Mpenzi, nimekuwa nikihudhuria semina mbalimbali kila mwaka tangu nianze kujitegemea. Semina hizi zimekuwa zikikuhubiri wewe na uzuri wako. Ninachoshukuru ni kwamba watoa mada hawakuwa wakiacha kueleza ugumu uliopo kukupata na kukutunza. Ni jinsi ulivyo wa gharama kubwa.

Kumekuwa na watu wengi wanaojaribu kukuelezea kwa namna mbalimbali. Wanasema upatikanaji wako unategemea na mtazamo wa mhusika mwenyewe. Mimi binafsi nimekuwa nikikubaliana nao lakini ukweli unabaki palepale kwamba yeyote yule anayejaribu kukuelezea bila kuweka neno PESA, HELA, FEDHA ndani yake anakuwa anauongopea umma. Una uhusiano mkubwa na hao ndugu zako niliowataja. Nisamehe kama nimekosea kuwataja.

Mpenzi, sijachoka kukufukuzia. Iwe kwenye barabara ya vumbi, lami au moramu, nitakutoa Nduki ili tu nikuweke ndani.

Wewe una uwezo wa kuishi na watu wengi kwa wakati mmoja. Simaanishi kwamba wewe ni Malaya La! hasha.  Ndio maana unaishi na Bill Gates, unaishi na Mo Dewji, unaishi na Bakhresa lakini bado na sisi nina uhakika hutatuacha na hiki kimuhemuhe.

Nimekubali kuwa mwaka uliopita haukuwa fungu langu au fungu letu. Lakini ombi langu kubwa ni kwamba usiipuuze Barua yangu ya Wazi kwako Mpenzi. Tunakuhitaji kuliko unavyodhani.

Nina mengi ya kuandika lakini acha niishie hapa kwani najua Hauji tu kiholela, unawajia wapambanaji. Kila mtu anakupenda MAFANIKIO. Nakupenda sana mpenzi wangu MAFANIKIO.

Ukishaisoma barua hii itunze kama kumbukumbu mpenzi wangu. Ili siku nikikupata usiwe na sababu ya kuniacha kwenye mataa.

Kiswahili, Mafanikio, Success


Elisha Nassary

History is a part of my story.

Comments (10)

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: