LAITI KAMA NISINGALIZALIWA BUBU

Nafungua kinywa changu ili niseme, niseme yale yaliyoujaza moyo wangu. Lakini nahisi uzito wa ajabu kwenye midomo yangu, taya zangu zinafunguka kwa taabu kana kwamba zimefungiwa kitu kizito. Najaribu kupaza sauti lakini ni kama vile koromeo langu limezuiwa, nahisi kama nimekabwa na jinamizi katika ndoto mbaya usiku. Kila ninavyojitahidi kutoa sauti yangu nizungumze ndivyo ninavyozidi kuumia. Nawaza ni kwanini mateso haya yote niyapitie ilihali mimi pia ni kiumbe cha Mungu? Ila kabla sijakufuru kuna sauti inanikumbusha kuwa hivi ndivyo nilivyozaliwa na nitabaki kuwa hivi milele. Nilizaliwa bubu nisiyeweza kusema lakini nikaweza kusikia, kuona na kufanya mengine mengi. Mungu hakuninyima kila kitu akanipa pia uwezo wa kuandika ili kuyatoa yaliyo moyoni mwangu.Laiti kama nisingalizaliwa bubu basi ningeyasema mengi sana ambayo kwa kiasi kikubwa huwa nashindwa kuyaandika.

Laiti kama nisingalizaliwa bubu ingekua vyepesi kwangu kuelezea mengi ambayo huwa nayapitia. Kuna nyakati huwa nabubujikwa na machozi na hata wanaponiuliza huwa nashindwa kuwajibu maana lugha ninayotumia ni ngumu kwao kuielewa. Kuna wakati huwa nashindwa kuelezea hisia zangu juu ya mambo kadha wa kadha maana huwa wanasahau hata kuniuliza kwasababu wakianza kubishana mimi huwa ni kama sipo maana siwezi kutoa sauti. Watabishana kuhusu timu yangu pendwa ya Arsenal na kuikosoa kisawasawa lakini pamoja na pointi nyingi nilizonazo huwa nakaa kimya kwani hawatonielewa.
Kuna siku mpenzi wangu alikua akilalamika kuwa anapata wakati mgumu sana kunielewa na anahisi pengine labda simpendi kwa dhati. Hapa ndipo nilipogundua kwamba katika ulimwengu ambao vipofu ni watawala basi anayepewa uwezo wa kuona ni kama amelaaniwa. Ninachojaribu kusema ni kwamba mpenzi wangu amezoea sana kuupata upendo katika maneno kuliko matendo hivyo matendo yangu kwake ni kama santana kumpigia gitaa mbuzi, yaani pamoja na ufundi wa santana kamwe mbuzi hawezi kucheza.

Ndugu zangu nao huniona wa tofauti sana japo hawawezi kunitenga maana damu ni nzito kuliko maji. Utaona tuu namna wanavyokwepa kukaa karibu na wewe mpige stori, sio makosa yao maana hawawezi kuielewa lugha yangu. Namshukuru sana mama maana kwa kiasi kikubwa sana yeye ndiye amekua msaada wangu tangu nikiwa mtoto mchanga kabisa. Aligundua kuwa nina tatizo pale tuu aliponizaa kwani manesi walimwambia kuwa pamoja na kwamba amejifungua mtoto mwenye afya njema ila ametoa machozi pasipo kilio. Uchungu wa mwana aujuaye mama maana kuanzia siku hii mama alitambua ya kwamba maisha yangu yote yatakua na changamoto moja kubwa, kwamba ningeumia au kuumizwa sana pasipo kujua namna ya kuonyesha uchungu wangu kwa nje. Siku zote mama aliamua kunipigania pale alipoona kuwa naonewa na alipaza sauti pale alipoona kuwa natamani kusema ila nashindwa.

Nililelewa na kukua katika jamii ambayo inaamini sana katika yale yanayooneka kuliko yasiyoonekana. Jamii ambayo ikiona mtu anamiliki gari basi itaamini moja kwa moja kuwa mtu huyu amefanikiwa kimaisha hata kama gari hili ni la mkopo. Jamii ambayo wengi wao wameshindwa kumwamini Mungu maana hanekani na kuamua kwenda kwa waganga wanaonekana na kuleta matokeo wanayoyaahidi. Kwa miaka kadhaa tuliishi na jamii ya namna hii bila kuwa na wasiwasi wowote lakini sintofahamu ilikuja baada ya jamii hii kuamua kuhamishia maisha haya mtandaoni.

Ilipokuja mitandao ikaunganisha vijiji vingi sana na kufanya viwe kama Kijiji kimoja kikubwa. Huku sasa maisha yetu ya kawaida yakaanza kubadilika na kuwa maisha ya kujionyesha kwa wengine kuwa sisi ni bora zaidi “show off”. Ikawa sasa badala ya kutembeleana tunatengeza tuu magroup ya WhatsApp na kila kitu kinaishia huko. Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba hata majina yetu ya kawaida tukaanza kuyabadilisha na kuwa na majina mapya ambayo tuliyaona kuwa na mvuto zaidi. Nilitamani sana kuongea na Rafiki zangu niliosoma nao juu ya hili lakini nani angenisikia? nani angenielewa? Yaani laiti kama nisingalizaliwa bubu sauti yangu ingewafikia wote hawa.

Sasa kwasababu jamii iliamua kuwa na maisha ya aina mbili yaani yale ya mtandaoni na yale ya mtaani tukaanza kujenga jamii iliyojaa wanafiki, watu wasioweza kusimamia yale wanayoyasema. Yaani kama nisingalizaliwa bubu ningekuwa Mchungaji Kanisani au Imamu Msikitini. Ningeyasema yote kwa sauti na wote wayasikie tena bila kupepesa macho au kuremba maneno. Ningesema kwa wote na wala nisingeweka matabaka, ningemsema Tajiri sawa na masikini bila kujali nani analeta sadaka kubwa zaidi. Ningekemea uzinzi unaofanywa na vijana kwa kisingizio cha kukwepa kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Ningesema pia kuhusu ndoa zinazofungwa nje ya kanisa au msikiti na kuvunjika mara tuu zinapopelekwa huko kwa ajili ya uthibitisho.

Lakini pengine nisingekuwa Mchungaji Kanisani au Imamu Msikitini. Pengine labda ningekuwa mwanaharakati, lakini sio mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake au wanaume bali mwanaharakati wa kutetea watoto. Watoto ambao leo wanakosa haki zao za msingi kwasababu tuu mzazi yuko busy na kazi. Watoto ambao wanashindwa kusema kinachowakuta shuleni maana wakirudi nyumabani mama nae amechoka na yuko Instagram anapambana kwenda sawa na dunia ya utandawazi. Watoto ambao wanazaliwa bila maandalizi hivyo kukosa wazazi wa kuwalea na kuishia daycare au kwenye mikono ya dada wa kazi ambaye yeye naye alikosa malezi bora. Ila ningetilia mkazo malezi ya mtoto wa kiume ambaye anasahaulika kwa kasi na kuonekana kana kwamba hana hatari ya kupata madhara lakini hatari ni kubwa kuliko tunavyodhani.

Pamoja na kwamba sina sauti ila naamini kuwa kalamu yangu inaweza kusaidia kufikisha ujumbe huu kwa walengwa. Sitoacha kuililia jamii yangu ambayo kwa kasi sana inaelekea shimoni lakini zaidi sitoacha kuandika kuhusu familia ambayo ndiyo msingi wa jamii iliyo bora. Mimi sio mtaalamu ila natazama, nafikiri, kisha naandika.

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,260 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: