MALI BILA DAFTARI, a short story

 

Roshi alikuwa kifua wazi huku akijipepea kwa kutumia fulana yake tegemezi ya Tigopesa licha ya kuwa hajawahi kufanya kazi Tigo wala kutumia huduma zake, sembuse ‘atume na ya kutolea’. Kiufupi tu Roshi alipewa fulana hii kama zawadi na imekuwa na mchango mkubwa kwenye kumsitiri. Fulana hiyohiyo leo imegeuka kiyoyozi. Kiza kilikuwa kimeanza kuifukuza nuru ya jua. Wimbo “Bao” wa Wagosi-wa-Kaya uliifanya safari ya Roshi kuelekea nyumbani kwake iwe fupi. Alikuwa amechoka kutokana na kazi yake ngumu ya kufyatua matofali.
Akiwa njiani bado mchovu, macho yake hayakushindwa kuangaza njiani. Dakika hii macho yake yalilenga kwenye bahasha iliyokuwa kando kando ya barabara.
Licha ya elimu yake ndogo, hakushindwa kutambua kwamba bahasha hutumika kubeba vitu au nyaraka muhimu. Ndiyo maana alianza kuiendea bahasha ile kwa shauku ya kutaka kujua je! Yaliyomo yamo?

Lahaula! Bahati ya mtende kwa Roshi. Bahasha ilikuwa nzito welikweli. Alikuta fedha ambazo kwa kuziangalia hazikuwa chini ya milioni 10.

Inatosha kusema Roshi alipagawa. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kutazama huku na kule kuona kama kuna yeyote aliyemwona. “Clear” hapakuwa na mtu maeneo yale. Kilichofuata alizima mziki kwenye simu yake. Kumbe mziki hugeuka kuwa kelele ukishashika hela!
Roshi alifika nyumbani akiwa mtu tofauti na yule wa muda mchache uliopita. Hakuwa tena mfyatua tofali. Alifikia kwenye kijumba chake na kutia hela zake benki. Yaani chini ya godoro. Sifa ya hii benki ni kwamba Panya husaidia kwenye ‘Transactions and Expenditure’
Kwa kasi ya umeme aliogea maji ya baridi na kisha akatupia viwalo vyake vya akiba vilivyobakia. Hivi kitaalamu huwa vinaitwa Kauka-Nikuvae maana alivifua asubuhi tu kabla ya kwenda kazini na sasa vilihitajika kuvaliwa tena. www.letswrite.co.ke
Alichota kiasi cha pesa kisichokuwa na idadi kisha akatembea kifua mbele hadi barabarani ambapo aliita bodaboda. Safari ilikwiva. Moja moja hadi maeneo ya Shara zilipokuwa Baa na Maduka ya nyama. Kwakuwa ni wikiendi, palifurika watu. Aliagiza bia raundi moja baada ya nyingine. Hazikuwa bia pekee bali pia na nyama kilo tatu kwa awamu tofauti tofauti. Kwa upande mwingine hii ilikuwa ni sherehe kwa wale wote waliohudhuria viwanja siku hii. Mwanzoni walitaka kumnyima huduma kutokana na tabia yake ya kunywa na kutolipa. Mara nyingine huleta vurugu kwa kukosa pesa za malipo. Lakini baada ya kuona mifuko yake imetuna waliridhia kumhudumia. Baada ya ‘kuwa bwii’ alirejea nyumbani kwake akiwa mweupeeee!
Siku zilizofuata, Roshi hakuwa mtu wa kutembea kwa miguu. Choo chake kilichozungushiwa mifuko ya nailoni kilipungukiwa harufu kwasababu hakikutumika muda mrefu. Roshi hakuwa mtu wa kukata gogo kwenye vyoo vya hovyo. Alikuwa akiita bodaboda impeleke hadi maeneo yenye vyoo vya kisasa vya kuflashi na kulipia. Madereva bodaboda walivuna hela kwake maana hakuwa mchoyo wala bahili. Raundi moja ya kumpeleka akaachie kojo la asubuhi kwenye vyoo vya kuflashi iligharimu si chini ya elfu kumi. Raha iliyoje!
Siku moja Roshi alipiga simu kwa mmoja wa wapiga dili wa msituni akihitaji silaha aina ya bastola ili aweze kulinda fedha zake. Haikuwa kazi ngumu maana waswahili walishasema ‘Penye udhia penyeza rupia’. Aliamini kabisa hakuna atakayemsogelea.
“Yani mshikaji wako siku hizi simwoni hata kazini haji tena. Ni kipi kimemsibu Roshi?”
“Bwana wewe, mhuni siku hizi haitwi tena Roshi. Anaitwa Roooshilingi. Anamwaga mihela tu kila kona anayopita. Hata chooni haendi kwa miguu. Anapelekwa town kukata gogo manake vyoo vyetu hivi vimemshinda.”
“Mamaaaa hehehehhe! ni Roshi huyu huyu ninayemfahamu mimi au mwingine?”
“Huyo huyo mfyatua tofali mwenzako. Sio Levo zako mzee. Anamiliki hadi chuma”
“daah ama kweli ndumba hizi”
Petro na Dunga walikuwa wanavuruga tope kwa ajili ya tofali huku Roshi akiwa Kiunganishi cha soga zao.
Kule kwa wanakijiji ndiko hasa stori za Roshi zilipamba moto. Si unajua tena maisha ya kijijini! Wengi hawakuacha kutamka neno uchawi midomoni mwao. Wengine walisema Free Mason wameingia rasmi kijijini kwao. Chanzo cha pesa za Roshi kilikuwa kizungumkuti. Sintofahamu hii wa kuitatua alikuwa ni Roshi pekee. Yeye ndiye kata kwahiyo siri ya mtungi aliijua peke yake. Kubaki na siri hii kulifanya wambea wawe watunzi bora wa hadithi zisizo na ukweli. Miongoni mwao alikuwepo Mimu ambaye Roshi aliwahi kumtongoza akamkatalia kwasababu ya hali yake. Jibu alilopewa Roshi siku hiyo baada ya kurusha chambo kwa pisi kali lilikuwa ni “Hebu nenda katafute kwanza hela upate hata ya kubadilishia nguo” INAUMA lakini ndio ukweli. Roshi hakuwa na kitu. Leo hii kibao kimegeuka na Mimu amekuwa msimuliaji mzuri wa namna Roshi alivyomwua ndugu yake ili apate utajiri. Jambo ambalo si kweli hata kidogo.
Mwonekano wa Roshi siku hizi ni ule wa “Kaka Habari” kutoka kwa warembo. Alijizolea umaarufu kwa wanawake wapenda Kitonga. Aliwashughulikia kisawasawa ndani ya hizi wiki chache.
Muda huu Roshi alikuwa amehamishia fedha kwenye akaunti nyingine. Sasa pesa zake zilikuwa shambani kando na kijumba chake. Huko aliamini mashambenga sio rahisi kumfikia.
Siku moja akiwa anapata chakula cha mchana kwenye hoteli fulani ya kienyeji, kwenye meza iliyosheheni vyakula na vinywaji; kuna nzi walikuwa wanarukaruka karibu na chakula chake na kumkera. Roshi hakuwa mtu wa kusumbuliwa na nzi kwenye starehe zake. Aliona wanamnyima amani wakati chakula kanunua kwa ajili yake tu. Alichomoa bastola ndogo kwa haraka na kuwafyatulia wale nzi. Cha ajabu hakuona maiti hata moja ya nzi. Zaidi ni kwamba alizua taharuki pale hotelini baada ya risasi ile kumpiga mmoja wa wateja mguuni na kumwumiza vibaya. Mshtuko uliotokana na mlio wa risasi ile uliwafanya watu walale chini bila ridhaa yao na hata wengine kupoteza fahamu.
Kufumba na kufumbua wanaume waliovalia sare za kutisha na virungu mikononi maarufu kama manyamwela walitua eneo la tukio. Hapa bado akili za Roshi zilikuwa hazijaanza sawa baada ya kugundua vimbwenga alivyofanya. Ama kweli Waswahili waliposema Shibe mwana malevya hawakukosea bali walisahau kitu kimoja, pesa nayo hulewesha. Bastola ya Roshi haikuwa imesajiliwa. Iliwahi pia kutumika kwenye uwindaji haramu ndani ya msitu wa hifadhi ya taifa ya Arusha kabla ya kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha.
Makosa ya wizi, uwindaji haramu, shambulizi la silaha kwenye eneo la umma, uhujumu uchumi na hata matumizi mabaya ya pesa kama uchanaji wa noti za kitanzania, ni baadhi ya makosa yaliyomkumba bwana Roshi ndani ya wiki kadhaa za utajiri wake.

Sijui niseme ndege ya pesa ilitua relini au Mali bila daftari huisha bila habari.

Hiyo ilikuwa hatima ya Roshi baada ya kunyimwa dhamana mahakamani.

Mwisho!


Elisha Nassary

History is a part of my story.

Comment

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,290 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: