MVUVI DIMBWINI

Kelele za magari ndizo zilizomuamsha toka katika kitanda chake kisichoeleweka mwanzo wake wala mwisho wake. Kitanda kilicho onesha dhahiri yake kimemaliza miongo minne bila ya josho wala marekebisho kwa zile chaga zake dhaifu zilivyojiishia, na mara hulalama kila kikitiliwa ubavu au kunyanyuka toka ubavuni mwake.

Kelele hizo ndizo haswaa humuamsha Mvuvi huyu akiamini kuzisikia kwake; mahoni na malalamiko ya mikwaruzo ya barabara pale madereva wanapoamua kukimbizana kuziwahi safari zao, nae hujinyanyua kitandani kwake kwenda kuzianza na kuzikabili harakati zake za kila siku.
Humchukua dakika mbili mpaka tatu tu kujiandaa, hata cha kujiandaa hakikuwepo kwa vile hakikuwepo kabisaa zaidi ya kusukutua maji mdomoni na kuyapuliza juu “fffuuu” na yale yaliorejea ardhini- akiamini ‘kila mpanda ngazi, hushuka’ – ndiyo yaliokuwa bahati yake kuyapatiliza na kuosha uso¬† wake. Hakujali kupoteza muda, saa hiyo ni saa kumi na moja unusu alfajiri, ndipo hujikongoja na kujivuta vuta taratibu kuelekea dimbwini; dimbwi lenyewe la msimu wa mvua tu, kiangazi lisionekane hata hata kwa dawa nae vivo hivo usimuone dimbwini nyakati hizo hata kwa dawa- aliendana nalo kama lilivotaka, akijisemea ‘ulipo tupo’.

Kadri alivokazana kukata hatua zilizomezwa na mipishano ya magari yalokuwa yakikimbizana ndivo nae alishikilia ndoano yake kwa nguvu aliyoinin’giniza katika Mtete mrefu, mkuu kuu lakini imara, katika nyakati kama hizi hakuna kitu alichokithamini kama Mtete huu na ndoano yake. Mkono wake wa kushoto alishikilia vyambo vyake, akijisongesha kuelekea dimbwini bila ya kujali kupeperushwa kwa shati lake mithili ya bendera nusu mlingoti wakati wa kipupwe na nusu kiangazi.

Alifika dimbwini mapema leo kidogo, akajisimamia kiasi ya dakika mbili, kashika kiuno chake, kichwani akijiuliza “leo itakuwa siku yangu kupata Kamongo au siku ya Kamongo kula chambo changu? Akaamua kujitosa rasmi katika uvuvi ‘rasmi’ – uvuvi aliourasimisha yeye mwenyewe kukidhi shida zake.

Ndoano yake alioipata kwa Shilingi Mia Tatu baada ya kupata ujira wake katika kuvunja kokoto – Machimbo ya Mawe- ikiwa tayari imenin’ginizwa chambo tayari kuizamisha katika Maji yalokwisha poteza rangi yake ya asili, yakitoa kijiharufu cha kukera na kukinaisha, lakini hapa ndipo Mvuvi huyu alipopatia riziki yake – harufu na bughudha za Maji, hazikumshughulisha- kwani ndiyo yaliomfanya kusukuma maisha yake taratibu kama si maisha kumsukuma tena msukumo wa kubimbirika mara kushoto, mara kulia na asiuelewe zaidi ya kwenda nao kama ulivotaka.

Akakusanya nguvu katika mkono wake wa kulia uliojazana kwa shuruba za kuponda kokoto na mawe baada ya kazi ‘rasmi’ ya uvuvi asubuhi. Akairusha Ndoano katika dimbwi, ikayaingia maji mazima mazima ‘chuuu’, maji nayo maji bila ajizi ikaipokea ndoano na kuimeza mpaka katikati ya tumbo lake, tumbo lililochanganyikana na tope zito lililotoa dhahiri ya rangi ya maji yale. Baada ya kuhakiki imefika penyewe akauchomeka Mtete wake kando, akisubiri windo lake linase – Kamongo.
Mvuvi akajituliza kidogo juu ya kijiwe chake cha kila siku wakati akisubiri Ndoano iteteme, akavua shati lake na kaptula yake iliyoraruka mapande sita, tayari kujitosa majini pembezoni mwa dimbwi bila ya kulishughulisha windo lake na akimakinika nalo kila sekunde, hii ndio ilokuwa ada ya Mvuvi huyu – baada ya kuhakiki Ndoano i majini, hujitosa majini kujiswafi na kutoa jasho la shombo na vumba, baada ya mihangaiko ya mchana kutwa na usiku wake baada ya kujiliwaza kwa Mama Muuza.
Hupiga mbizi kadhaa katika dimbwi hilo na anapomaliza hujirudi katika kijiwe chake anapoota Jua mwenyewe akiamini ananururishwa na Vitamin D huku akisubiri Ndoano itikisike kuashiria kunaswa kwa windo lake. Husubiri bila kuchoka bila ya kun’goa unyao, seuze kiwiliwili chake kilichoanza kujichokea kwa suluba alizopambana nazo mpaka sasa uzee nao unamgongea hodi.
‘Mtafutaji Hachoki, Akichoka Kapata’ mara Mtete wake ukatikisika, ukiangaishwa huku na kule- Kamongo kanaswa-. Akakurupuka, baada ya kiusingizi kumpitia, tabasamu jembamba akalitoa pembeni ya mashavu yake. Akaushika Mtete wake, akajaribu kuuvuta kwa nguvu, ikambidi kuongeza nguvu kidogo tofauti na siku zote, akashtuka “leo nimenasa nini, jamaani? akasimpa kiasi, akavuta, akavuta, akafanikiwa kuutoa majini, laa haulah!! Akastaajabu, akatumbua macho na kupanua mdomo vyote kwa pamoja – haikuwa Komongo, bali likamongo- hakuwahi kupata Kamongo mkubwa kiasi hiki katika uvuvi wake siku zote.

Hakuchoka kuhangaishana nalo, mara juu, mara chini – kala mweleka, chiinii- kasimama, bado kashikilia Mtete wake, kan’gan’gana Kamongo asimchoropoke na hakuwa tayari kupoteza windo lake – bora afe, maana windo lake ndilo lililomuhakikishia kuishi kwake.
Akafanikiwa, akamvuta mwambani, Kamongo akarukaruka, akatapatapa, Mvuvi akamkamata barabara, Kamongo akatatarika huku na kule, Mvuvi akakenua kwa furaha kichwani mwake alishakwenda Sokoni, kwa Mama Lishe, akamuuza Kamongo wake kwa bei ya kutupa, akaifumbata pesa yake, akaichikichia katika mifuko ya kaptula yake, akajigamba na kutamba, sasa amekuwa ‘mnene’ kwa pesa ya jasho lake, akapiga picha yupo kwa Mama Muuza, akiwalewesha na kuwastarehesha rafiki zake akitekeleza msemo wake aliukariri vizuri ‘KAZI NA BATA’. Akashituka bado yupo dimbwini na Kamongo wake mikononi, akatoa kicheko cha kuridhia na kuridhika kwa kupata windo lake, akamchukua Kamongo wake, akaondoka zake.
**************************************************
Mvuvi Dimbwini, ni hadithi ya kubuni yenye kuakisi Maisha ya raia wa kawaida yenye mafunzo mbalimbali kadri ya Msomaji atavyoamua kuchagua cha kujifunza, kwani kwa hakika ‘Dunia Haimalizikiwi na Mafunzo’.

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: