NINACHO CHA KUSIMULIA (Simulizi ya Kweli)

Utangulizi

Naandika simulizi hii nikiwa Arusha, Tanzania.

Nimeamua kumzungumzia bibi huyu aliyeakisi maisha ya wakati uliopita kwa mazuri na mabaya. Lakini mimi nitamkumbuka kwa mema mengi.

Bibi yangu alifariki 2018 akiwa na umri wa miaka 104 (Japo hana namba ya NIDA). Hatukuwa na shida sana lakini alikuwa akitembea umbali mrefu na kuomba chochote kwa watu aliokutana nao barabarani. Endapo ukimnyima au ukiwa huna basi hakuridhika na alitukana matusi makubwa sana.

Bibi alikuwa akifurahi sana endapo ukimpatia walau Tsh 200 kwaajili ya ugoro. Au ukimpa Tsh 500 basi angenunua maziwa tumpikie chai ya jioni kwasababu nyumba ilikuwa ya mbao yenye baridi kali kama ijulikanavyo wilaya ya Meru-Arusha.

Bibi alikuwa anapenda sana wageni ila sharti uje na sukari hata kilo1 au nusu kilo,au kamzigo kokote. Kwa Kimeru tunaita “Kilambo” au ikiwa ni kamzigo ka kuning’iniza tunaita “Kilolo”. Bibi alikuwa anatukana watu ambao ni uzao wake lakini hawakuwa wakimtembelea kwa zaidi ya miaka miwili na kuendelea.

Mama na Bibi

Mama yangu alikuwa binti yake wa mwisho, mtu wa karibu kuliko wote kwani yeye ndiye alijua bibi anakula nini anakunywa nini na analala wapi. Cha kushukuru ni kwamba pamoja na baridi yote bibi hakuwa mgonjwa wa baridi. Sijui ni kwasababu ya kuwa mzawa!

Mama alipitia changamoto nyingi kuna wakati alilia kutokana na yale aliyokuwa akifanyiwa na bibi. Nyumba ilikuwa ndio jiko humohumo, Bibi alikuwa anapenda kupika na ilifika wakati akatenga mafiga yake tofauti hakutaka tena kushirikiana na mama. Kuna wakati walikorofishana wakiwa jikoni, kisirani cha bibi hakikuwa mchezo.

Chakula kikubwa kilikuwa ni Ugali wa Mboga za majani. Lakini kadri siku zilivyokwenda uzee ulizidi, akawa anakula kidogo sana,chai kwa wingi,Wali angalau aliweza kula sababu ya ukosefu wa meno.

Mimi na Bibi

Niliishi na bibi udogoni mwangu. Hii ni baada ya mama kuhamia kwa bibi nikiwa mchanga pindi walipoachana na Baba. Pamoja na kuomba kwake, bibi hakuwa mchoyo. Ulikuwa ukimchotea maji bombani na kumletea atakuzawadi japo kakitu kadogo. Alikuwa akinipa Tsh kadhaa mara kwa mara nilipomsaidia jambo nami nikafurahia kumiliki hela(si unajua utoto) Lakini kufurahia kwangu vihela vidogo ni kwasababu mama hakuniruhusu kabisa kushughulika na vitu vinavyoingiza pesa kama watoto wenzangu hadi namaliza Shule ya msingi. Mpaka leo huwa nawaza Labda mama aliamini kuniruhusu nijiingize kwenye masuala ya pesa kwenye umri mdogo kungeniharibia stara na maisha kiujumla au nini ulikuwa wasiwasi wake? Yote kwa yote nimeshakuwa mtu mzima na nikagundua kwamba kila mzazi ana njia yake ya kuhakikisha malezi bora kwa mwanae.

Cha Kufurahisha Kuhusu Bibi

Kama sikosei Bibi aliwahi kusafiri mara moja tu kwa gari kuelekea Moshi mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania.

Yeye ni miongoni mwa wanakijiji wachache wa kipindi hicho kupata hii nafasi kwasababu tu mjukuu wake alisoma akawa mwinjilisti KKKT. Wengine huko kijijini hawakuwahi kupanda gari kwenda safari ya mbali hata mara moja mpaka wanafariki. Inafurahisha? Hahah! Ndiyo maisha.

Cha ajabu bibi alikuwa akiapa kwamba hatokuja kupanda tena gari maishani mwake kwasababu ya ule mto wa kutisha aliouona kwa wakati ule. Katika kutafakari na kuunganisha mambo nilipokuwa mkubwa nikaja kugundua ule mto uliomuogopesha bibi ni mto Kikafu. Upo kwenye barabara kuu ya Moshi kuelekea Arusha. Na kweli aligoma kabisa kwenda kwa wanae walioishi mbali baada ya kupata maisha maana aliuogopa ule mto.

Akiwa kwenye miaka ya 80-90 bibi aliwashangaza wengi kwa ile kauli yake ya “Niny nfoo ndi. Na nkonu nfoo fuwa tikapaa na mariko eekaa” akimaanisha “Mimi sitokufa. Na siku nikifa mvua zitanyesha na mito itafurika”
Hapo Ukimbishia useme atakufa lazima akurushe jiwe au rungu lililopo karibu naye.

Mshangao

Pamoja na matusi lakini bibi alijiita mwalimu wa Sunday School. Alikuwa akifatana na watoto Jumapili asubuhi kwenda kusali mpaka pale aliposhindwa kimwili.

Mpaka leo najiuliza kwanini alizingatia sana tarehe na muda japo hakuwahi kumiliki saa ya mkononi?. Akitazama angani aliweza kujua ni saa7 au saa9. Ilikuwa lazima aniulize leo ni juma ngapi? Hapa alikuwa anaweka sawa rekodi zake bila shaka.

Bibi alikuwa na BIBLIA chakavu japo hakujua kusoma. Alikuwa akikutana na mtu anamwambia “nisomee Wakorintho hapo”. Au anataja kifungu kidogo alichowahi kusikia kwenye Biblia. Mfano wa mistari aliyozoea sana kuitaja ilikuwa ni “Waheshimu sana baba yako na mama yako”.

Sikitiko

Ilifika mahali kulala kwa mama ikawa tabu maana bibi usiku mzima alikuwa anaimba tu na kelele tupu. Ila ilimlazimu kuzoea kwasababu ndiye mama pekee aliye naye.

Pamoja na kuwa na wajukuu na Vitukuu zaidi ya 32 kuna wakati bibi alikula kwa kusuasua. Hii ilipelekea kumpenda mtu pale anapomletea kitu na kuwatukana wasiomjali kwa mali zao.

Maisha yalisonga. Siku moja akiwa anarudi nyumbani toka kwenye mihangaiko yake,aliteleza akaanguka anguko dogo tu (hakuvunjika) umbali kama mita 60 kufika nyumbani. Ila kutokana na uzee bibi alianzia palepale kuumwa miguu akawa hatembei tena bali kukaa na kulala kitandani tu. Waliokuwa wakimtoa nje aote jua ni mama pamoja na wake za wanae.

Huduma zote alipewa na watoto-wakwe zake lakini kadri siku zilivyokwenda walimwachia mama yangu majukumu yote kama awali. Ikiwemo kufua nguo na kumwogesha bibi ilhali mama alikuwa mlemavu wa kidole kimoja cha mkono wa kuume.

Hatimae lile wazo lake la kutokupanda gari lilivunjwa baada ya kupelekwa hospitali alipozidiwa. Kwenye vipimo vya madaktari Hakukutwa na tatizo lolote ila alipewa dozi ya dawa za kutuliza maumivu na kurejesha nguvu. Wiki kadhaa zilipita hatimae asubuhi moja alilala tu na hakuamka tena. Alifariki na ndipo akapanda gari kwa mara ya tatu kuivunja ahadi yake. Aliaga dunia. (R.I.P Ndekingiyo).

Ajabu

Mwezi Septemba Siku1 kabla ya maziko mvua ilinyesha kubwa Kata nzima ya Songoro na watu walishindwa kuvuka mito isiyo na madaraja. (Rejea kauli yake) “Sitokufa, na siku nikifa mvua zitanyesha na mito itafurika”. Hakutuhadaa au aliona mbele…sijui.

Kama hujajua,basi nikuambie Bibi yangu hakuwa na akili nzuri (Tatizo la Akili) ila kuna Mengi ya kujifunza kwake ambayo yalinifanya niandike makala hii kama kumuenzi na kuwafunza watu wengine kuwa ‘dhahabu haipatikani mahali pasafi’. Kiufupi maisha yetu ya kijijini yananipa sababu na nguvu ya kusema NINACHO CHA KUSIMULIA.

a mother's love, Be live in people's hearts even if you dead


Elisha Nassary

History is a part of my story.

Comments (12)

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: