UANAFUNZI, Mwanzo wa stori za maisha.

UANAFUNZI raha bwana!

Haijalishi ni mwanafunzi wa ngazi gani ya elimu, kuna mengi ya kusimulia katika uanafunzi.

Sina uzoefu wa uanafunzi katika nchi zingine ila naamini kutokana na yale ninayo yaona na kuyasikia, uanafunzi wa hapa unashabihiana sana na uanafunzi wa kule. Hii ni mbali na mfanano wa kiuchumi au kiutamaduni.

Hivi unakumbuka uanafunzi wako ulikuwa vipi pindi ukiwa shule ya msingi, sekondari au chuo? Una kipi cha kusimulia kiwe chema au kibaya? Unaweza kuweka maoni yako pale chini kabisa baada ya kusoma huu “Utopolo”.

Kuna mengi sana huyajui au unayajua lakini napaswa kukukumbusha kuhusu uanafunzi. Hebu twende sambamba nami.

WAJUA

Yunifomu ndilo vazi, ila lisipo fanyiwa mafekeche na kutiwa manjonjo halinogi. Mara modo, suruali bila mapindo na mbwembwe zingine kibao. Hii ndiyo raha ya suruali ya shule bwana!

JARIBU

Kama wewe ni mwalimu mwenzangu, hebu mtangazie mwanafunzi wako kuwa avae shati la mikono mirefu, halafu subiri mrejesho. Wiki ijayo atapita-pita huko ajuako, atakopa buku ilimradi apite kwa fundi nguo alikate mikono liwe na mikono mifupi. Huu ndio uanafunzi, mwanzo wa stori za maisha.

Au basi mtangazie avae shati la mikono mifupi  keshokutwa atakuja na tomato mpyaaaaaa! Ya mikono mirefu na atavalia sweta muda wote ili usimwone. Ole wako usubiri akiwa kwenye gwaride la asubuhi umwambie avue sweta. Atakimbia. Huo ndio uanafunzi, mwanzo wa stori za maisha.

Au basi mwambie avae viatu vya ngozi kama sheria za shule zisemavyo. Ataiba hata raba/bajaji ya ndugu yake ilmradi awateke wenzake darasani kwa mitupio. Huu ndio uanafunzi, mwanzo wa stori za maisha.

Mwanafunzi wa kibongo bwana usipomkagua usafi utakoma mwenyewe kwa huo uchafu. Maana haitakuwa kero kwake, itakuwa kero kwako mwalimu na wenzake. Huo ndio uanafunzi bwana.

SIRI YA WAZI

Leo nakupa siri. Wanafunzi ndilo  kundi la watu linalo ongoza kwa kukariri nyimbo za kidunia. Wengine huita bongo fleva endapo ni ya kitanzania. Wewe mwenyewe unakumbuka nyimbo za kina P Square au Westlife ulizokuwa ukiandika kwenye kile kitabu chako kidogo cha kumbukumbu. Sijui ulikuwa unaenda kumwimbia mpenzi wako ama vipi, mimi hainihusu.

Wanafunzi wanaongoza kwa kutaka vitu vya thamani japo sio wote wapatao. Hii huwa ni chachu itokanayo na vile waonavyo. Wanafunzi wengi wako katika hatua za mwanzo za ukuaji hivyo huathiriwa na mazingira waliyopo. Mara nyingine baadhi yao hugeuka wezi. Uanafunzi, mwanzo wa stori za maisha.

Ukimwekea ukuta mwanafunzi ni kosa kubwa sana maana hata kama hana ishu yo yote mjini atatoroka ili tu, akukomoe.

Yule wa kike haoni shida kuwa mpenzi wa mwalimu, mwanafunzi mwenza, mpishi, mjumbe, mlinzi au hata Mkuu wa shule ilmradi maisha swafi na kukwepa baadhi ya adhabu.

HATIMA

Hatima ya haya yote huwa sio nzuri. Wengine huishia kutia/kutiwa mimba wakiwa wadogo kinyume na sheria, wengine huacha shule, wengine huishia kuwa wahalifu.

USHAURI

Wazazi, waalimu na wafanyakazi wengine ni mihimili muhimu. Hawa wana mchango mkubwa sana katika malezi ya watoto wanafunzi. Pengine hata watu wazima. Tushirikiane kuhakikisha malengo ya kizazi kijacho katika elimu yanakuwa timilifu na yenye manufaa kwa watu na taifa kiujumla.

Wenu katika usukumaji wa gurudumu la elimu, mwalimu Mshamba.

Student


Elisha Nassary

History is a part of my story.

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,290 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: