UCHOCHORO

Asikudanganye mtu, katika Ulimwengu huu hakuna Nchi, Mji, Wilaya, Kata, Kijiji au hata Mtaa unaokosa kichochoo au kichochoro… Hahahaa!! Unashangaa, usishangae ndo ukweli huo. Hata huko wanakosema ni Dunia ya kwanza kulikopangwa na kupangika kwa Miji na Mitaa yake, ambako ukisimama mwanzo wa mtaa mpaka mtu wa mwisho wa mtaa kwenye nyumba zenye kaya zaidi ya mia mbili nako kuna Vichochoro vile vile na huku kwetu nako, nako kumepangika vile vile tena kumepangika kwa namna yake, nako Vichochoro¬† vipo tena vipo mpaka ambako hapakustahili kuwa na hivo vichochoro.

Huwezi kuzunguka Mtaani kwako? Wacha mi nikuzungushe kidogo uone vitu vitamu vitaamu vinavyopatikana katika vichochoo vyenu – vichochoo ambavyo vimeundwa kwa migongo ya nyumba zenu nyingi za mgongo wa tembo, au mbavu za Mbwa, tena zimepauliwa ki,slope tu kurahisisha maisha, maana ni bora tusinyeshewe na tujihifadhi tu, mambo ya mabati sita na kenchi mia, nenda huko waliko wale wasosalimia kila wakipita kisa tu wanatembelea ‘makalio’ Masikini Akipata….. Utamalizia mwenyewe!!!

Ebu, tuanze na kichochoro chenu, nasema chenu tena cha hapo mtaani kwenu, tena ndio cha nyumba yenu. Nikuulize kwanza, ukibanwa na mkojo ghafla, unaenda wap? Hahaha!! Unashangaa tena, usishangae, ni kichochoro chenu ndio kinatumika kama Choo cha dharura. Si kwako peke yako, hata kwa yule rafiki yako anaejipitiza tu, mara ghafla haja ikambana, hakuna pahala pakwenda zaidi ya kujibana katika kona ya kichochoro chenu, ataachia vitu hapo iwe ni vikubwa au vidogo, ndio hivo tena hakuna malipo, katoa udhia wake, huyooo kenda zake.

Nikuulize tena, hivi chemba za vyoo vyenu ziko wapi, tafadhali hapa siwagusi wenye vyoo vya ‘chubwiii’ – najua ushanielewa, ila kwa kuwa wajifanya ni wa kule kwengine wacha nikwambie “vyoo vya shimo”, umeelewa sasa? Sawa, turudi kwenye hili ninalolijua kuhusu kichochoro chenu huku ndiko chemba zenu mmezielekeza, eti mnakimbia harufu, harufu ipi zaidi ya ile ya choo cha dharura mkibanwa? Najua mmeziweka huku ili wakati wa mvua iwe rahisi kutapisha na kupeleka mizigo itakayokwenda na takataka na mabiringibiringi ya mvua za masika na vuli. Usishangae nimejuaje, kwani si ndo kichochoro chenu. Hahahaa!! Subiri hapo hapo.

Bado niko na wewe, usiondoke tafadhali maana huku ndiko kwenu. Ushawahi jiuliza wale jamaa wa kupuliza ‘cha Arusha’ ooouuhhoo, siku hizi wanasema ‘cha Iringa’ ndo kiko sokoni, eehhe, ushajiuliza huwa wanapulizia wapi? Kiukweli hakuna sehemu nzuri wanapenda kama katika Vichochoro vyenu maana huku ‘wazee wa kipira’ au ‘mamwera’ hawafiki sio kwamba hawawezi kufika, hapana, yaani hakufikiki, maana mpaka wafike kichochoroni kwenu, lazima wapite kijiweni kwenu na vile tunavyowapenda kabla hawajawafikia, tushawaambia tayari, wakifika hawakuti mtu, harufu tu. Hahahaa!! Unafurahia kwenu sio? Tena huku, usijaribu kupita zaidi ya saa mbili usiku, usiseme sikukwambia, tena ujue huku ndiko kuna roba za mbao, bisibisi, mabeto na hata viwembe – huku viko nje nje, yasije yakakukuta. Nshakwambia tayari.

Leo kuna miadi ya kuonana, kuna watu washakubaliana ya kukubaliana, na wamekubaliana kuridhiana, kukutana, unadhani wanakutana wapi? Hahaha!! Ni hapo hapo nyuma ya nyumba yenu, kwenye uchochoro wenu. Huku si Baba, Mama wala Kaka hawawezi fika, na si hao hata yule jirani yenu hawezi jua kama Mke au Mume wake wanaweza patikana huku, ukweli ni kwamba huku ndiko makutano yenu rasmi, tubambiane haraka haraka tena usishangae ‘kumalizana’ kabisaa, wanasema ‘fasta fasta’ – uchochoro hutoa faragha hiyo na huwasitiri bila khiyari. Ukimtuma binti yako au kijana wako iwe sokoni au dukani, akachelewa na usimuone barabarani, usihangaike, pita vichochoroni, usishangae kumkuta katulia, katulizwa, hakumbuki alichotumwa hata ukimuuliza.

Ukikimbizwa, Kumbuka Vichochoro’

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: