UJINGA WA MBASI: Januari alivyotupa salamu za Stamina!

Hii ndio Januari S2, 2020; Januari ya kawaida iliisha, tukaingia Januari S2 na ndio tunafunga hesabu yake. Ni kama ‘series’ za simu vile, Samsung S1, S2, Iphone 6, 6+ au iPhone 7. Ndio ilivyo buana, Januari ni ndefu sana kuliko mwezi wowote katika siku 365 na zaidi.

Unaingia paap! umeshakula mshahara ulioingia Disemba 20 kwenye likizo na sherehe, unaingia mtandaoni kujipooza, unakutana na kauli ya mtangazaji Gadner G. Habash kuhusu mwanae wa kike, mrembo na msanii wa bongo flava, Malkia Karen awe na ‘sugar daddy’ ili amtunze. Kama mwanahipapu Stamina alivyoimba kwenye ngoma yake mpya; unaruhusiwa kushangaa, kama kuna ambaye anawaza ‘asiwaze.’

Stamina kwenye video ya Asiwaze

Ni mtangazaji mkongwe na mwenye ushawishi mkubwa kupitia kituo cha Clouds FM, Gadner G. Habash akafunguka ya moyoni kwenye ‘interview’ na Zamaradi na kusisitiza kuwa anatamani mama wa binti akate bili ndio binti atapata akili, “ Mimi ningetamani awe na mtu mzima mwenye umri kama wangu, sugar daddy ili amtunze sababu watu wenye umri kama wake hawawezi kumuelewa, wala hawawezi kumsaidia kwa chochote.’’

Mtandaoni wanasema ni kiki ya ngoma mpya ya ‘Tabu’ binti aliyoachia, wengine aah mzee wake anatengeneza mazingira gani kwa binti, ina maana umri ule hawezi kujitafutia, wakati ana mpaka digrii kutoka pale katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)?

Gadner na bintinye Karen

Kuna ule msemo wa kiingereza usemao, ‘Words belongs to speaker/ writer but interpretation belongs to audience.’ Maneno ni mali ya msemaji ila tafsiri ni mali yetu, hivyo ujinga wangu unanituma kuwa yawezekana labda Gadner yupo sahihi.

Nasisitiza tena ‘labda’ ila hakuwa na mtiririko sahihi wa mawazo, na upande wa pili ni kuwa; inashangaza baba kunena yale kwa mwanae, ukizingatia binti ni msomi wa digrii kabisa anaweza kujipambania maisha yakaenda, japo ajira ngumu.

Je, angekuwa hana pakushika au hana kipaji? Ila ndio kusema mwanamke yapaswa ahudumiwe? Sawa ahudumiwe, lakini si kwenye ‘engo’ ya baba meneja wake!

Ujumbe kwa binti ‘asiwaze’ buana kama mke wa Stamina, maana kuna akili za kuambiwa nawe changanya na zako, lakini ujinga wangu unanituma kuwa, mbona baadhi ya mabinti wengi wanafanya hivyo kimjini mjini wanasema ‘kuji-position’ ili maisha yaende, na yanaenda.

Mpaka mafeministi na wanaharakati wakaongea, kuna kakundi kangu pendwa ka’wasapu, binti mmoja machachari akasema, ‘Ni sahihi, kuhaso na kula kwa jasho tunajitakia tu, tunaenda kinyume na maandiko, sie tuliandikiwa tuzae kwa uchungu buana.’ Nikacheka kwa staha tu!

Mwambie anayetaka kumwelewa baba meneja Gadner, asijisumbue; yaani ‘asiwaze’ kabisa, yeye anasema hajaeleweka na msimamo wake uko palepale.Januari na vimbanga vyake!

Ulikuwa umenuna sasa unaanza kutabasamu, maisha ndivyo yalivyo, Januari pekee ndio mwezi wenye ‘series’ kama simu au ‘muvi’ yenye part 1 na 2. Maisha ndivyo yalivyo, ada za watoto, kulipa kodi ya nyumba, madeni ya 2019 na namna ya kuanza mwaka mpya ni balaa, ndio maana Njaanuary inatuchanganya!

Mambo kama hayakupangiliwa vizuri Januari S2 anazidi kuyavuruga vizuri, hichi ndicho kile kipindi inasemekana urafiki wa wengi huvunjika kisa mikopo. Halafu watu wanaonana wabaya; kwa Stamina sio mkopo, yeye kamfungukia ya moyoni mkewe ‘asiwaze’ kabisa kwa kuweka hadharani kuwa ndoa imevunjika kwakuwa washaonana wabaya. Anasema mkewe akija msibani atafufuka ampige vibao!

“Mwambieni yule dogo aliyechezea klabu ya Simba, kutembea na mke wangu asijione ameshinda, Mimi samaki mapenzi yangu yana shombo, kaka yake nishakula ruksa kutoa vyombo.”

Hii fasihi tamu ila haijajificha. Haya ni baadhi ya mashairi yaliyoko kwenye ngoma ya Stamina iitwayo ‘asiwaze’ aliyomshirikisha Atan. Anasisitiza yeye ndio wa kwanza, lakini ndio hivyo kashaondoka, kashaumizwa, ama kweli ndoa ni chungu kama Januari vile.

Mwanamuziki Stamina wakati wa ndoa yake

Huku na huku kuna wadau wakamuuliza msemaji wa Simba, Haji Manara, vipi umesikia wimbo huo? Akajibu kwa kusema Stamina amweke hadharani mchezaji mwenyewe.

Watu ni wagumu sana kuelewa, kama ilivyo mwezi Januari, Stamina kasema, aliyekuwa mchezaji wa Simba. Dogo gani ameondoka Simba?
Mie naona watu wazima tu Emmanuel Okwi, James Kotei, Haruna Niyonzima n.k au ni utenzi ‘dogo’ ili azidi kufanya mambo yawe magumu?

Janauri 13 Simba anafungwa goli moja katika fainali ya Mapinduzi Cup na Mtibwa Sugar, Mwekezaji wa Simba ana-tweet kuwa atabaki na cheo cha mwekezaji si mwenyekiti wa bodi tena, anamaindi kulipa mshahara unaokaribia bilioni 4 kwa mwaka halafu matokeo yanasuasua, japo asubuhi yake akajirudi. Inauma sana, ndio Januari hii, mwambieni MO kama ya Stamina wetu tu,‘asiwaze.’

Wadau wanakwambia ni laana la Stamina kwa aliyekuwa ‘dogo’ wa Simba kutembea na mkewe, inachekesha sana, ndio Januari S2 tulivyoianza hivyo.

Mkali wa kufokafoka na mwenye mistari kwenzi, Shorobwenzi kutoka mji kasoro bahari, Morogoro, Stamina alifunga ndoa kikatoliki mwaka 2017, alichukua mwaka na siku kadhaa ikasemekana wameachana na mkewe, akafunguka mwenyewe Januari hii kwa kupigilia msumari kuwa alikuwa kuwenye mahusiano lakini hajui yanahusiana na nini?

Ila ukiicheki Januari ilivyo ngumu ndio unafurahia raha ya kuwa Tanzania, unacheka kidogo!

Hii imenikumbusha kuna kamsemo kanasema, eti umesomea Mahusiano ya Umma ila kuna mtu mmoja anakuchanganya kwenye mahusiano, ndio uelewe kabisa kama kuna ambaye anawaza sana ‘asiwaze’ achange tu karata vizuri kabla ya kuingia ndoani.

Ukisikiliza kwa umakini unajua jinsi gani jamaa alivyoumia akaamua atuwekee kwenye mashairi mapito yake na ndio inavyokuwaga, na lazima ngoma ‘ihit’ buana, imekuwa ‘ontrend yutubu’ kwa siku kadhaa.

Unakumbuka ‘Inauma sana’ na ‘Sitaki demu’ za Juma Nature dongo kwa mwigizaji Sinta enzi hizo mwanzoni mwa miaka ya 2000 au juzi kati Mondi kwa Wema au Barnaba kwa mkewe. Ndio wasanii walivyo, hasira wanamalizia kwenye ‘booth’.

Hayo ndio mambo ya Januari, nimetulia hapa kwenye kiduka cha mangi nikiisikiliza hii ngoma ya Stamina ‘asiwaze’ nikinywa sharubati yangu ya ukwaju hapa, ni ngoma nzuri yenye mafunzo ya ndoa. Ngoja nijifunze mie nikipambana na Njaanuari yangu

#Januari, #Salamu, Gadner, Karen, Stamina


Peter

PETER MMBAGA is the content and digital media consultant found in Dar es Salaam, a wordsmith with poetry pen name 'Mbasi', maybe you can call him 'jack of all trade' or 'writing savvy' in writing arena with his creative writings ranging from; newspaper features, copy writing, creative strategic planning, music composing, blogging, content marketing and poetry.  For him 'writing' is business and passion. Connect with him, Twitter @Mbasi  & Instagram @mbasiofficial

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,260 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: