UJINGA WA MBASI: Makamba ni ‘Twitter Sweetheart’, wewe ni nani mtaani?

Mambo vipi huko wajameni? Kama kawaida kijiwe kipo ‘on faya’ kwasababu mambo nayo ni moto pia, sie tunajivunia kijana mwenzetu kutambulika na Makamu wa Rais kuwa ni Twita Sweetheart, tujivunie kipi zaidi?

Habari imetrendi hiyo, katika siku ya kuzaliwa kwa Makamu wa Rais, mama yetu Samia Suluhu Januari 27 ambapo mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye naye akazaliwa kesho yake, Januari 28 akampa ‘wish’ mama kama ilivyokuwa kwa wengine.Mama akamshuru kijana wake na kummwagia sifa kuwa anasikia ndiye ‘Twitter Sweetheart’.

Wakati nafika tu kijiweni nakuta Mangi hajachangamka, Wakishua kaagiza safari yake nusu saa imepita haijaletwa, mabinti anavyowachangamkiaga hapa dukani, mpaka wanamuita ‘Sweet Mangi’ leo kawanunia.
Nikajisemea moyoni lipo jambo, nagundua baadaye kisa ni Benki ile kuzuia fedha kwa ajili ya elimu kisa mabinti waliobeba mimba kudaiwa kutorudishwa shuleni mpaka huduma zinaenda ‘slow’ dukani kwake, inasemekana wanaharakati ndio chanzo!

Wakishua akaanza kijembe, yaani ungekuwa kiongozi ninge-bet ‘Piga bet’ ili utumbuliwe.
Mkushi akajichekesha huku akisema, Watanzania kwa kwenda na ‘trend’ marehemu Kobe Bryant mcheza kikapu wa Marekani aliyefariki kwa ajali ya helikopta, kuna kadada kanasema sauti ya Kobe akiimba ni noma.

Mangi akadai sasa wewe kuacha ujadili vyenye mwelekeo unajadili kujichekesha hapa wakati wanaharakati wamezuia huko.
Wakishua akamjibu kwa kusema, si yaleyale tu mbona wanaopelekewa nao ‘wamezuiliwa’ huku? Mangi akalalamika, sasa wanamkomoa nani? Wakishua akamjibua akasema nao wanamkomoa nani?

Mkongwe akajibu kwa kusema nyie mshalewa mapema sana, na Mangi utalewaje, utatuuziaje bia?
Mbasi Rasta na lafudhi yake ya kichaga akasema makosa ni kitu cha ajabu sana kama Mungu anasamehe, mbona wengine hawasamehewi halafu wanamuamini Mungu?

Mkongwe akampiga kijembe Rasta, si ufungue kanisa na uzee wangu niwe mzee wa kanisa, Nguya na uhasibu wake atakuwa mweka hazina wa kanisa. Mangi wewe huruhusiwi hata kusogelea mimbari maana hatukuamini kwenye hela usije ukasema tufunge duka la kanisa, halafu ukatugeuka!
Mwalimu wa St. Kayumba akadai, mwaka juzi 2018 ilizuiliwa, leo tena inazuiliwa tena, sio sawa.

Mbasi Seng’o leo karudi mtaani na vibe la kutosha sana tangu alivyoenda kuhesabiwa Moshi Desemba 2019. Akachangia huku akiwa na majonzi akisema, tukiwa sekondari 2010 nilimpa binti mimba, lakini leo hii ni mhasibu wa benki!
Grupu wa admini wetu wa wasapu akasema, wataendelea kwenye mifumo mingine, sio kwamba ndio hawasomi kabisa.

Mbasi Oba akasikitika kwa kusema, unajua haya mambo ni changamoto sana, tufungue ‘pandora box’ unaweza wakaruhusiwa ikaonekana ni ka’fasheni hivi si nitarudi tu shuleni mabinti wakajiachia tu. Ukiwakataza ndio hivyo tena!
Mkongwe akashikwa na kigugumizi kidogo kabla ya kuongea, Wakishua akasema, Mangi mpe maji madogo huyu kwanza, maana akaianzaga kigugumizi ujue anamwaga ‘vyointi’.

Mkongwe akadai ninyi vijana hamjui mengi sana, mmenizoea sana hapa kijiweni eeh? Haimaanishi ukiwa mkali tabia mbaya ya wanao itakoma ukiwa mzazi. Watoto hawa wanapitia kipindi cha ‘foolish age’ ni kipindi kigumu. Wanafanya makosa lakini haiidhinishi kuwa wahukumiwe kutokana na makosa yao.

Mkushi akasema wewe unavyosema hivyo unadhani ndio itawasadia, wengine wanajitakia wenyewe kuna vigodoro utawakuta huko.

Mbasi Kitokololo akamkatiza Mkushi kwa kusema, hawajui, imetolewa kama angalizo na kuwakumbusha hawa mabinti kuwa shule kwanza. Wazo la viongozi ni positivu, wanajua wanachokifanya!

Mkongwe akasema kuna wale waliopata nje ya unayosema kama kudanganywa, kubakwa au kurubuniwa kutokana na umbali mrefu wa kwenda shule?

Mkushi akadai, hapa cha msingi kingine iweke tume maalum na sheria zitungwe kuwajua wale waliopata kwa hali hiyo, si ushahidi upo kwa daktari na polisi, halafu baadae wapewe kipaumbele.

Nguya akasema, mkiwasema sana mabinti hamjengi, kwakuwa kama elimu haina mwisho hata elimu ya uzazi tusichoke kila siku kuinena, kama unaona imetosha tusingekuwa na shule na vyuo vikuu. Kila siku ni siku ya kujifunza tutoe ujinga wetu.

Mkushi akasema, waliozuia wanaelewa wanachokifanya, hii ni kuwafanya wafikirie umuhimu wa elimu zaidi, nyie mnaona kama wanaonewa.

Mkongwe akasema, mtoto kwa mzazi hakui kabisa tusichoke kuwaelimisha. Kwani makosa ni kupata ujauzito pekee, kuna watoro shuleni na wengine wenye tabia mbovu mbona wanarekebika.

Nguya akasema, yote tisa, lakini Mkongwe hivi ile miaka 30 kwa baba wa mtoto, halafu mama naye ndio hivyo tena? Mkongwe akasema, ndio sheria hiyo, unataka nisemeje mie leimani?

Mkushi, akamjibu ila hii mijamaa nayo buana kwa wanafunzi si bora iende maeneo ya wale ‘wa usiku’ ambao ndio wameamua maisha yao ndio hivyo, unaenda kurubuni vitoto vya shule kweli?

Wabasi kijiweni wakiendeleza gumzo, mara Mbasi Kai akaingia na boda yake huku ameachia mziki mkubwa ukiimba, ‘Nenda kwanza shule halafu mambo mengine yatafuata’. Ni ‘Baby Candy’ kibao cha kitambo kutoka kwa mkongwe Dully Sykes.
Mkongwe akasema, wanaume wote wangewafikiria kama Dully kwa watoto wetu tungefika mbali?

Mkongwe akasema, si mnapendwa kuitwa ‘Sweetheart’ nyie, kuna maeneo unaitwa ‘Sweetheart’ mpaka unafurahi mwenyewe sio vitoto aisee.

Mkushi akauliza, ‘Tanzania Sweetheart’ vipi hapo? Mbasi Oba akasema kama Watanzania wenyewe wameridhia mbona poa tu. Mbona mabinti hapa mtaani wameridhia kumuita ‘Sweet Mangi’ mwenye kiduka chake?

Wakishua akadakia, wewe hapa mtaani unaitwa nani? Ungemuwazia binti wa mwenzio ni wako tusingefika huku.

Nguya akasema mabinti ofisini kwetu wanamuita kiongozi wetu ‘Sweet CEO’. Kwa uungwana, ndio tunatakiwa tuwe hivyo. Hawa mabinti waache wakue jamani!

Mzee wa Twita akasema, Makamba yeye anaitwa ‘Twitter Sweetheart’ jamaa anastahili kweli ni mtu wa watu, jamaa yupo ‘positivu’ sana.

Mkongwe akadakia haya wenzangu na mie, nyie ni kina nani huko maofisini, nyumbani na mtaani, au ndio ma-sweetheart kwa wanafunzi?

#Makamba, #TwitterSweetheart


Peter

PETER MMBAGA is the content and digital media consultant found in Dar es Salaam, a wordsmith with poetry pen name 'Mbasi', maybe you can call him 'jack of all trade' or 'writing savvy' in writing arena with his creative writings ranging from; newspaper features, copy writing, creative strategic planning, music composing, blogging, content marketing and poetry.  For him 'writing' is business and passion. Connect with him, Twitter @Mbasi  & Instagram @mbasiofficial

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,290 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: