UJINGA WA MBASI: Nchi zilizoendelea wanakanyaga mafuta au umaskini wetu ni mtaji tija?

Shalom waungwana? Kijiweni ni masikitiko tukikumbuka ya huko Moshi kwa vifo vya kukanyaga mafuta, Mangi kaweka bendera nusu mlingoti hapa dukani kwake.

Tangu mwaka uanze lililomfurahisha Mangi ni Samatta kusaini Villa pekee.

La mafuta linapoozwa na kuombewa ‘wallet’ zetu. Wakishua anamuuliza Mangi, Wachaga imekuwaje kukanyaga, si tunajua mnasaka hela?

Mkongwe akasema, Wakishua wewe hujui mambo ya imani eeh? Wakishua akajibu si kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo bayana yasionekana.

Mbasi Kai akasema, nyie mbona mnataka kutuchanganya na neno, heshimuni basi.

Mkushi akasema neno lazima liheshimiwe ila lazima tuzichunguze roho, imeandikwa kwenye biblia ila siukumbuki mstari. Mungu alitupa utashi ndio tuutumie kutafakari ku-control hisia!

Ghafla mwalimu wetu na Mkushi aliyetufundisha somo la dini (Divinity) tulivyokuwa sekondari, Mwalimu Emmanuel Maqway akapita tukasilimiana, Mkushi akamualika kijiweni atupe madini kidogo.

Wakishua akasema afadhali anajua somo la biblia wengine hapa ni walevi tu. Hivi kukanyaga mafuta imekaaje hii Mwalimu, yawezekana waliokanyaga wameingia paradiso moja kwa moja?

Mwalimu Maqway akadai, mimi sio Mungu sijui, ninachojua tuliumbwa kwa neema na tutakombolewa kwa neema. Hivyo paradiso ni neema, tutaiona kwa neema!

Mwalimu wa St. Kayumba akasema, tumuombe Mungu awalaze pema peponi.

Mbasi Nguya akamuuliza, hivi kukanyaga mafuta na kuombea ‘wallet’ bila kufanya kazi kunatendeka jambo?

Mwalimu Maqway akasema, mkiwa na imani bila kujishughulisha ni kazi bure. Kuhusu mafuta kwa tafsiri ya biblia sio mpaka ukanyage au upakwe, ni jambo la kiroho zaidi.

Mfano alichofanya Yesu kimwili (physically) kitafsiriwe kiroho pekee, kifo ni kutenda dhambi, Yesu alisema Lazaro amelala (alikufa akiwa mwema) wakimwambia amenuka, hivyo hatuhitaji body resurrection (ufufuo wa kimwili) katika gharama ya ukristo lazima mwili utaabike, hakuna mwili unaoneemeka kirahisi katika ufufuo wa kiroho (spiritual resurrection).

Kumfufua Lazaro, Yohana (11:17-41) haukumaanisha ni kimwili bali kiroho. Kwani Lazaro aliishi milele, si alikufa tena?

Nguya akamsema mzee hapo umetuacha kidogo, tufafanulie tuelewe kirahisi?

Mwalim Maqway akaendelea kunena, ni mtaji wa tija wa watu kufanikisha malengo fulani tu. Je, ingekuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa au walioko bize kufanya ugunduzi na teknolojia, kukanyaga mafuta kungewezekana?

Wakishua akasema, mzee anatuchanganya na falsafa zake sasa biblia si ile ile mzee kwani kuna nini?

Mwalimu Maqway akaitikia, ni ile ile changamoto ni jinsi jamii mbalimbali zinavyoweza kutafsiri si kingine, kwani lugha za asili ya biblia ni Kiyunani, Kiamharic na Kiebrania, lakini tuna mpaka za makabila ya hapa kwetu.

Na neno lenyewe ‘tafsiri’ lina ukakasi kama huzijui lugha hizo za asili ukalidadavua kimazingira, elimu ya dini, wakati, imani, uzoefu,  utamaduni, tafakuri n.k

Mzee Mkongwe akasema, ndiyo; changamoto ni tafsiri. Taifa letu lina umaskini ambao unaumiza mpaka fikra zetu, kukanyaga mafuta ni rahisi kutendeka  kuliko Uingereza, Israel yenyewe. Tunaongozwa na hisia kuliko tafakuri!

Rasta na lafudhi yake ya kichaga akasema, aisee umeongea kitu mzee, hili suala ni kweli mwambie mtu pale New York au London akanyage mafuta si anakuchapa vibao mzee.

Mkushi akasisitiza, tena huko Beijing au Tokyo wajuba wanawaza kugundua magari mapya baada ya Toyota na IST soko bwerere Afrika waambie wakanyage mafuta, woi hawatakuelewa.

Mwalimu wa St. Kayumba akadokeza, au ndio tunaangamia kwa kukosa maarifa?

Mwalimu Maqway akaendeleza neno, kwenye kitabu cha Yohana, Yesu amesema yeye ni mpakwa mafuta lakini hakuna sehemu alikanyaga mafuta.

Maqway akaendelea kunena kuwa, ukikumbuka Yesu alipobatizwa akazamishwa kwenye maji haikumaanisha lazima uzamishwe kilichopo ni roho yake kutakaswa. Hao wafia dini (martyrdom) wangekuwa wa kwanza kukanyaga!

Mkushi akasema, hata umpe mtu mafuta ya korie useme umeyaombea bila kuwa na imani ni kazi bure.

Mwalimu Maqway akatupa tafakuri zaidi, tafsiri ya theolojia ya mafuta ni kuijua kweli, maana yake kunukia manukato. Ni lugha ya picha, ina maana mng’ao, mvuto au harufu ya kimungu ukimuona tu unastuka unajua ndiye. Sawa na Samweli baada ya kumpaka mafuta Daudi mwana wa Yesse (1 Samweli 16-23).

Mkushi akasema, ni kweli hata Yesu alivyokuja mbona wengi walistuka kuliko manabii waliokuwepo, ule Umungu wake tu nadhani.

Mwalimu Maqway akasema, ndiyo hivyo sasa prosperity gospels (injili za juu ya neema ya mwili) zimezidisha sana kuhubiri mafanikio ya mali na miujiza kwa maneno matamu kuacha injili ya uhalisia (gospel of reality).

Mbasi Nguya akasema, wapigwe marufuku, makanisa hayo yapungue kidogo, ni mengi kuliko hata viwanda tupate ajira vijana,  watu 18 ni wengi inawezekana asilimia kubwa ni kinamama na watoto.

Wakishua akadai, China, Czech na Sweden ni kati ya nchi ambazo raia wake wapo chini ya asilimia 30 kwa kufuatilia dini lakini maendeleo yao yakoje?

Mzee Mkongwe akadai, uchumi mdogo na ndio tunaongoza kwa makanisa kwenye nchi zetu zaidi ya asilimia 80, angalia Nigeria au Kongo makanisa mengi na vita bado haziishi.

Mzee wa Twita akatuonyesha video huko mtandaoni yule mama akipiga meza pale mjengoni wakati mbunge yule akisema mbunge mwingine auawe kisa suala kuiandika benki ile barua hela za wanafunzi wale zisije.

Mkushi  akasema, mama huyu si mchungaji, sasa siasa na uchungaji wapi na wapi? Akiwa kwenye siasa anaweza kusapoti mtu auawe jamani?

Mwalimu Maqway akasema, siasa ni mfumo wa maisha, hata mwanafalsafa wa kale Aristotle alisema ‘human is politically animal’ yaani kiasili mwanadamu ni mwanasiasa kwa ‘kuongea’ na ‘kuongoza’. Huwezi tenganisha mwanadamu na siasa au siasa na dini kwani uongozi ni siasa. Na kwenye dini kuna viongozi na mama yule ni kiongozi.

Mwalimu wa St. Kayumba akasema, sasa waumini pale wanamuonaje na si ndio ‘rolu modo’ wao?

Nguya akasema, fuata neno langu, usifuate matendo yangu.

Mwalimu Maqway akasema ni binadamu kama sie wenye madhaifu, tusome sana vitabu vya dini sio kuhadithiwa. Tuweze kujiombea wenyewe kabla ya kuombewa lakini cha muhimu tufanye kazi, kwani hata Muumba alifanya kazi siku sita, ya saba akapumzika wewe ni nani uombewe ‘wallet’ yako halafu hufanyi kazi?

Kijiweni leo tukawa tumepigwa neno la tafakuri, kabla ya Maqway kuondoka akatuacha na mshangao kuwa kwa sasa duniani kuna dhambi mbili za kusingiziana ambayo tunazifanya sana, kumsingiza shetani na kumsingizia Roho Mtakatifu nje ya utashi wa kibinadamu.

Hatukumuelewa, Mkushi akauliza kivipi Mwalimu yaani  shetani tumsingizie?

Mwalimu Maqway akatupa somo kuwa, dhambi ya kumsingizia shetani, ukikamatwa umezini, kuiba, au kuua unajitetea shetani kanipitia na baadae mtume au mchungaji wako anamsingizia roho mtakatifu kwa kukuelezea  kuwa nunua kichupa cha mafuta kwa elfu ishirini roho mtakatifu atakuponesha, huoni mmewasingizia hapo?

 

Mbasi wako,

Peter Mmbaga

 

 

 

 

 

 

#KukanyaMafuta, #Kupakwamafuta, #mtajitija


Peter

PETER MMBAGA is the content and digital media consultant found in Dar es Salaam, a wordsmith with poetry pen name 'Mbasi', maybe you can call him 'jack of all trade' or 'writing savvy' in writing arena with his creative writings ranging from; newspaper features, copy writing, creative strategic planning, music composing, blogging, content marketing and poetry.  For him 'writing' is business and passion. Connect with him, Twitter @Mbasi  & Instagram @mbasiofficial

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: