UJINGA WA MBASI: NIDA acha tulalamike, ndicho tulichonacho!

“Ndugu mteja namba yako imefungwa kwa kutosajili kwa alama za vidole….”. Kinachofuata ni lawama dhidi mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kwa mujibu wa mamlaka ya mawasiliano (TCRA) mpaka kufika Jumatatu ya Januari 20 ambayo ni siku ya mwisho ya zoezi, laini milioni 21.4 zilikuwa hazijasajiliwa, laini milioni 27.3 sawa na asilimia 56%, ndizo zizokwishasajiliwa.

Mjinga mie kama kawa niko kwenye kiduka cha mangi na wajinga wenzangu tuliotofautiana viwango vya ujinga wetu, stori zinaendelea. Mangi anasema, Mbwana Samatta kwenda Aston Villa ya EPL akitokea Genk Ubelgiji ni bonge la hatua kwa mpira wetu, kijiwe kizima kikaitikia, hakika Samatta anatuinua sana.

Mbasi Wakishua ghafla anatokea na kudandia mada, Sio poa, euro milioni 10.50, hela ndefu mwanangu Mbasi. Nikamjibu, vipi unapatikana kwanza? Nimemuuliza hivyo kwasababu Disemba 31 tukiingojea 2020 alilalamika ameshazimiwa wakati bado Januari 20 aliyoiongeza Rais wetu haikuwa imefika. Alidai, ‘‘Wanna wish my mom happy new year but they have already locked my sim card”. Akimaanisha kuwa anapaswa ampe heri ya mwaka mpya mama’ake ila washamfungia laini.

Akajibu, sio poa, sijui itakuwaje? Vipi kama una tigopesa au M-pesa yako? Mangi akamjibu TCRA wamesema fedha zitakuwa salama kwa miezi mitatu kama hujafanikiwa kurejesha laini wasiliana na kampuni husika ya simu!

Dakika nyingi hazikupita Mbasi Rasta akaingia kijiweni na povu zito, “Nimetokea NIDA, foleni ni hatari. Tunapoteza hela mingi sana Daslamu, ukianzia kwenye foleni barabarani.”

Baadhi ya watu wakiwa kwenye foleni ya kupata kitambulisho cha Taifa

Nikadakia kwa kumwambia, “Mwendokasi imejengwa, ‘flaiova’ ya TAZARA na ya Ubungo serikali inaendeleza ujenzi.” Mbasi Rasta akazidisha kihoro na lafudhi yake ya kichaga kwa kusema, ‘Unaona sawa kitu NIDA wanatufanyia? Unaenda mapema unatoka jioni ati, hupati hata hiyo nambari, acha kabisa!

Wakishua akamjibu ‘Come down, man’. Wakishua mbwembwe kutumia ung’eng’e sio kwasababu akipiga bia mbili tatu, ameishi Ulaya kitambo, Rasta akamjibu, “Biashara zinalala Mangi”.

Mbasi Rasta ambaye ni wakala wa mkubwa wa miamala ya fedha wa kampuni za simu akaendelea kulalamika, Itakuwaje mamilioni ya kuwasiliana na kutuma miamala? Kiasi gani kitapotea, hela imelala tu? Woii! Kamisheni (commission) ndio ‘baibai.’

Mzee mkongwe kijiweni akaibuka baada ya kupoa sana leo, “NIDA watachelewesha kwenye uchumi wa kati anaouhubiri Rais wetu.” Rasta akamjibu, Nimesema tunapoteza hela mingi hamkunielewa, muda unaokaa foleni utakuwa umeingiza shingapi?

Mkongwe akatafakari kisha akasema, au wahudumu wa NIDA ni wachache? Wakishua, akamjibu labda wafanyakazi hewa walikuwamo, you never know!

Mbasi Nguya akaingilia kwa fujo, kwakuwa ni mhasibu anajua mambo ya uchumi ikabidi atupeleke darasani. Hiyo ni kama illiquid money (mali zisizoweza kuuzika kwa sasa kama vile hisa au hati fungani n.k) haizunguki kabisa, watu milioni ngapi hawatatuma wala kupokea hela? Cha msingi hapa watumie busara zaidi, unajua TRA watakosa kodi pia?

Nikamuuliza kivipi hapo? Kabla ya kunijibu Mbasi Nguya akamwambia Mangi, ‘Konyagi ndogo’, Mbasi Wakishua akamchokoza, maliza safari, umevurugwa na NIDA eeh?

Mashine ya kusajili laini kwa alama za vidole

Akacheka akitushangaa, Nishajisajili mapema, si dakika za mwisho kama mstaafu JK. Mzee wa Twita akachomekea, mstaafu ali-twiti akionyesha picha akijisajili tarehe 19, siku moja kabla ya kuzuiliwa!

Ujinga wangu ukanituma kuwa mjadala wa msingi wa mapato unapotezwa, ikabidi nimrudishe kwenye reli Mbasi Nguya. Nikamchapa swali, serikali itakosaje kodi?

Akasema tuulizeni, ‘sisi ndio wataalamu’, Mzee mkongwe akamzodoa akisema, “Tupeane maarifa tupungazane ujinga tulionao, hata wewe ni mjinga kwenye elimu ya ‘soshoweki’ aliyosomea Wakishua, huijui.” Nikapigilia msumari, mweleze huyo!

Mbasi Nguya akajichekesha huku akifafanunua, “Enewei, unalipia vipi luku kwa simu? Hata kabla hatujamjibu akaendelea. Malipo ya maji, mifuko ya jamii kama NSSF, WCF, NHIF n.k yote hiyo itaathirika.

Ticha wa shule ya St. Kayumba mwanakijiwe msomi pia, akadakia, malipo kwenye mashirika na taasisi za serikali,uhamiaji, kituo cha uwekezaji, malipo ya maji na umeme hufanyika kupitia mfumo wa kielekroniki wa Government ePay Gateaway (GeGP) na yote haya ni kupitia huduma za kifedha za mabenki kutumia simu ya mkononi (sim banking).

Huduma ya benki mkononi kupitia simu janja

Mbasi Nguya akaenelea kumwaga ‘vyointi’. Makampuni ya simu inawezekana yamepoteza, waliokopa nivushe, tala, voda songesha, na tigo niwezeshe itakuwaje?

Mkongwe akatikisa kichwa akisema, NIDA, nani anakurudisha nyuma? Mkushi akameza funda la bia huku akinena, CAG aliyasema kwenye ripoti kuwa utendaji kazi wa mkandarasi uangaliwe, pia NIDA waharakishe utengenezaji vitambulisho.

Mzee wa Twita akasema, inasemeka tupo kwenye orodha ya walioekewa vikwazo kama Iraq, Iran na wengineo. Nguya akasema, kwahiyo Wakishua safari ya Marekani imeisha? Wakishua akajibu kinyonge, “Sio poa, let wait mpaka Januari 27 wataweka wazi hiyo ni tetesi Wabasi.”

Mkushi akasema, sio lazima kwenda majuu, mmesikia wa Maliasili wamemtia kidole jichoni? Hii ni kwa mujibu wa akaunti yake ya Instagram hii hapa (akituonyesha). Ni ujumbe mrefu, baadhi ya maneno yanasema, “Aliyenitia kidole jichoni sasa akae sawa. Naanza kujibu mashambulizi. Aliyetaka vita sasa ameipata!

Mkushi akakazia, anadai waandishi wa habari wa gazeti fulani wanamchafua. Mzee mkongwe akasema watoto wa mjini wanasema ‘katoa povu’, yamemfika kooni, analalamika.

Nguya akasema unataka afanyeje, yeye kama Mtanzania? Ukizidiwa unalalama tu, hicho tulichobakiwa nacho!

Watu wakaanza kuulizana, kivipi? Mzee mkongwe akasema, ‘maji yashakworogweka nyie’. Tukiwa tumetahamaki mkongwe ana maana gani, Mangi akaanza kuingiza viti ndani.

Kijiwe kikaanza kupukutia; nikaanza kusikia jamani kesho wana, mara mwingine napatikana S.L.P 30304 Buza kwa Lulenge!

 

Mwandishi wa makala haya, PETER MMBAGA ni mshauri (consultant) wa maudhui, mahusiano ya umma (PR) na mitandao ya kidijitali. Anapatikana kwa baruapepe:  petermmbaga29@gmail.com

#malalamiko, #NIDA, #UjingaWaMbasi, #usajulialamazavidole


Peter

PETER MMBAGA is the content and digital media consultant found in Dar es Salaam, a wordsmith with poetry pen name 'Mbasi', maybe you can call him 'jack of all trade' or 'writing savvy' in writing arena with his creative writings ranging from; newspaper features, copy writing, creative strategic planning, music composing, blogging, content marketing and poetry.  For him 'writing' is business and passion. Connect with him, Twitter @Mbasi  & Instagram @mbasiofficial

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,290 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: