UJINGA WA MBASI: Tusipokumbuka mazuri yako, tutakumbuka hata ‘uno’ lako!

Katika mihangaiko ya kusaka ugali naingia maskani nimechoka sana lakini inabidi nijongee kijiweni ‘nika-refresh’ na kubadilishana mawazo kidogo. Kitaifa tuna mijadala tofauti tofauti; kuna hili, mara hujakaa sawa kuna lile mpaka ile isiyo na kichwa wala miguu.

Ujinga wetu unatufanya tuwaze sana maana haijulikani lipi lishikwe au lipi liachwe, kwa yote yana umuhimu wake. Ukilisahau hili, utakumbuka lile na usipokumbuka zuri, utakumbuka baya!

Nafika kwenye kiduka cha Mangi, kijiwe kinasikitika na nyuso zinawaelemea, nikawasabahi nikisema, Wabasi mambo niaje?

Wakaitikia kwa bashasha lililopoa mpaka nikawaza vipi tena? Sikuelewa kinachoendelea, lipi linawasibu, la mheshimiwa ‘yule’ kusikikia kuwa anataka kuuawa, huyu kujiuzulu au yule mwingine ofisi yake kufungwa na ‘nywila’ asiingie ama kuna kipi mtaani?

Si unajua Watanzania ni ndugu, baya au zuri tunashikana, ndivyo tulivyofundishwa hata Mbwana Samatta kusainiwa EPL tumefurahia sote!

Ikabidi niulize maana sio kawaida yetu kutokuwa na ‘vibe’ kijiweni. Mzee mkongwe akasema, Ngeba haajaonekana toka juzi, ila hayupo kazini pia. Wamemwachisha kazi au kaacha kazi, hatujaelewa?

Wakishua akajibu Ngeba hana jeuri ya kuacha kazi. Kwanza, anamkubali sana bosi wa ile kampuni ukizingatia bosi wake ni muadilifu, mchapakazi na ni sawa na baba’ake kwakuwa aliwahi kumfundisha pia. Nani asingependa kuwa chini yake?

Nikasema, ndio maana hajaonekana kijiweni mpaka leo? Kabla hawajanijibu chochote ‘grupu admin’ wa kundi letu la ‘wasapu’ akatutuonyesha habari za Watanzania waliokamatwa wakiwa Sauzi bila utaratibu sahihi.

Mzee wa Twita akadakia, hiyo habari ‘ina-trend’ vijana 30 hivi. Mkongwe akadai, wanasaka fursa si mnajua ajira mtiti. Ila tuacheni utani makamanda walitenguliwa tenguliwa jamani, Arusha Ilala na Temeke!

Ticha wa St. Kayumba akakolezea, unaikumbuka 2018 alivyoingia tu, alivyowashusha vyeo wale askari, hivi ajali ziliisha? Kuna wale wa Zimamoto na Uokoaji walijitambulisha bila neno ‘Uokoaji’ mwisho wakatimuliwa kwenye kikao? Yule Kamishina aliyezuiliwa kuingia kwenye kikao Mbeya kwa kuchelewa dakika 1 tu, kikao kikianza saa 5 kamili asubuhi.

Rasta akasema, huwezi jua buana ndio ilipaswa iwe hivyo katika miongozo na majukumu, kwani ushawahi kumilikishwa V8 yenye pleti nambari inayoanza na ‘W’ wewe?

Mkongwe akasema, vijana hata kwa mujibu wa sheria kujitolea kwenye taifa lenu hamjaenda, hamjui tu vile vyeo vinavyosotewa mpaka kuja kuvaa jango au gwanda tu ujue ni msoto wa nguvu.

Mbasi Nguya akasema, watajitambulishaje ‘pleini’? Ndio maana nakwambia tutam-mis ninja kwa kusimamia utamkwaji kamili wa vitu vya msingi. Namkubali sana, anajiamini na msimamo anao, alimwambia CAG kama ikithibitika ukweli wa kashfa ya ufisadi wa sare za polisi angevua nguo!

Mjinga mie nikawaza nikasema ndio maana kijiweni anakubalika sana, si bure kwasababu ya misimamo yake isiyotingishwa.

Matukio ya kupotea kwa watu na shambulio la Lissu alisema hata waliompiga risasi Tupac huko Marekani 1996 hawakupatikana mpaka sasa na baadae kudai kwanini wasimkamate muathiriwa na dereva wake. Lakini kuhusu yule mwandishi alisema, “Sisi hatutafuti watu waliojipoteza kwa sababu zao za kimaisha”.

Mbasi Nguya akasema matukio ya kupotea kwa watu yamepungua hivi karibuni, kiasi fulani anaondoka pametulia, naamini wamethibitiwa.

Nikawaambia Wabasi, Jeshi letu lipo vizuri, lilikuwa suala la muda la watekaji kubanananishwa.

Mzee wa Twita akadai kuwa kati ya waheshimiwa ambayo walikuwa wazalendo na waaminifu kwa chama chao ni yeye. Alikuwa anatembea na ilani ya uchaguzi, nakutamani mpaka akifa azikwe nayo buana.

Rasta akaongea kwa lafudhi yake ya kichaga, tuongee la msingi, hizo trilioni sio uhujumu aisee? Mkongwe akajibu vijana tuyaache, tutaona yatakavyokuwa. Wakishua akasema, ‘perdiem’ dola 800 sio poa Wabasi. Ni nyingi!

Mkushi akaropoka, kwahiyo ashakuwa ‘removed’ kwenye kundi la ‘wasapu’ la Baraza? Tukaanza kucheka kidogo maana tulikuwa kama wafiwa, mkongwe akatukatisha kwa karipio. Ndicho cha msingi ulichoona? Mitandao ya kijamii inawaathiri vijana sana.

Mkushi akasema ‘kausha’ huku akituonyesha moja ya video za mheshimiwa akimpiku Mose Iyobo wa ‘dabliyusibii’ kwenye uno. Mzee mkongwe akasema yawezekana alikuwa ‘ngoma coy’ enzi zake huyo.

Ticha wa St. Kayumba akasema, moja ya majukumu yetu walimu ni kutazama vipaji. Kipaji anacho na ni mtu anayekufurahisha akiongea hata vitendo vyake. Alikuwa haboi ‘samutaimu’. Kucheza ni kitu alichokipenda!

Nguya akasema, changamoto ya Watanzania wengi wanaona mauno hadharani ni kukosa staha, ni ujuzi tu. Kama huwezi kwanini useme wenzako wanajidhalilisha?

Mkongwe akasema, kuna wanaoishi kwa kucheza, acheni ‘kidomodomo’. Huyo Mose Iyobo wa muziki wenu wa kizazi kipya si anaishi poa na mwanamke mzuri wa matawi ya juu, mbongo muvi kama Aunt Ezekiel angemzalia jamani? Au kwasababu ‘ninja’ ni mheshimiwa?

Mzee wa Twita akatuonesha habari ya mhe. Meya wa jiji akipata joto ya jiwe kwa kutimuliwa kikaoni, kunyang’anywa gari mpaka ofisini kuwekewa ‘nywila’.

Mkongwe akasema, kuweni muyaone wanangu haya mambo ni magumu kueleweka kabisa. Nani mbabe hapo haina ulazima. Wananchi wanataka maendeleo.

Mkushi akasema, maisha tunapita, walioumizwa naye wanajisikiaje? Mkongwe akasema vijana msijifanye watakatifu, kuna madhaifu pia ya kibinadamu katika utendaji tuyavumilie, japo yakizidi ni kero inahitajika busara sana hasa uongozi!

Mkongwe akaendelea kumwaga busara kwa kusema, “Kila binadamu ana eneo lenye nguvu na udhaifu kwenye maisha, kifupi ukiondoka unawaachia kitu, mazuri yataangaliwa lakini kuna kukwazika na udhaifu wako uliowaumiza hautofutika daima.”

Kijiwe kikasema hakika alikuwa mtu wa watu, kuna muda alifanya tutabasamu. ‘Tutam-miss’ sana, ndiyo maisha hayo. Ni kupanda na kushuka tu.

Wakishua akasema, ‘He was true ninja’. Nakumbuka kipindi kile bungeni kabla ya kuanza kuendeshwa kwenye pleti namba inayoanza herufi ‘W’ aliwachana mawaziri akisema anabidi avae kininja ili asiwaonee huruma kwa kuwa ni chama chake.

Ndipo mkongwe akanena kwa kusema. Tusipokumbuka mazuri yake, tutakumbuka hata ‘uno’ lake!

 

PETER MMBAGA ni mshauri (consultant) wa maudhui, mahusiano ya umma (PR) na mitandao ya kidijitali. Anapatikana kupitia; petermmbaga29@gmail.com

#mzuri, #UjingaWaMbasi, #uno, tutakukumbuka


Peter

PETER MMBAGA is the content and digital media consultant found in Dar es Salaam, a wordsmith with poetry pen name 'Mbasi', maybe you can call him 'jack of all trade' or 'writing savvy' in writing arena with his creative writings ranging from; newspaper features, copy writing, creative strategic planning, music composing, blogging, content marketing and poetry.  For him 'writing' is business and passion. Connect with him, Twitter @Mbasi  & Instagram @mbasiofficial

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,290 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: