Usiku Umeendelea sana

 

Usingizi ulikua ukininyemelea kwa mbali, mchanganyiko wa kahawa na limao haukutosha kuhimili nguvu zake.Jumbe za ‘whatsapp’ zilizidi kuingia kwenye simu yangu janja,kundi sogozi la darasa lilizidi kutuma jumbe za hapa na pale, nyingi kati ya hizo ikiwa ni ubashiri wa mitihani ambayo ilikua inakaribia,niliichukua simu yangu na kuipangusa kuelekea kulia kuzifunika jumbe zile kwani sikutaka kuzisoma kwa wakati ule.Nilishtushwa na vishindo vilivyosikika nje ya dirisha la chumba changu,kwa haraka niliwahi kwenye kiambaza kuzima swichi ya taa ya chumba changu.Niliendelea kusikia kilichotokea nje,niliyoyasikia hayajuzu kuandikwa katika kisa hiki.

Chumba kidogo kisichokua na ubora stahiki,kilitosha kunipumzisha na kuniandaa kwa kila asubuhi ijayo.Joto,fujo za majirani na runinga ya dirisha langu vilikua vihoja vilivyotosha kwa ushindani.Dirisha la chumba changu lilipakana vyema sana na uchochoro uliopitisha waendao kwa miguu kuvuna juhudi za mikono yao,na kuwarejesha wenye kazi za usiku katika uangamivu wao.Ni katika jiji hili ambapo wapo watu wa aina mbili tu walioishi maisha mazuri yaani;waliokula kwa jasho la nyuso zao na waliokula kwa vumbi la visigino vya wengine.Kijana kutoka paa la Afrika sikuzoea kabisa maisha niliyoyaona katika jiji hili,maisha ambayo watafutaji walitafutwa na watafutwa kutafuta,yaan ni patashika.

Jamii ambayo haikujali hisia za wengine wala kutazama mambo ya wengine ilikua imechipua sana mithili ya miche kati ya konde lenye mbolea.Jirani zangu ambao nilipakana nao vyumba hawakua watu wa hamasa,salamu tu ilitosha kumaliza siku yetu pengine hata wiki kama itatokea hatukukutana tena.Jirani yangu wa chumba cha kulia alikua kijana wa mambo mengi,niliahirisha kusoma mara kadhaa kwa fujo zake,wakati mwingine niliyoyasikia kutoka chumba chake yalinitoa nje kupunga upepo.Njama,uhalifu,uhuni yalikua mambo yaliyofika kirahisi kwenye runinga ya dirisha langu.

Nikiwa najisomea usiku sana,mara kadha nilisikia sauti ya nyimbo za kusifu na kuabudu kutokea kanisa lililoko jirani.Sikuwahi kufahamu kanisa hili liko wapi kwani nilijikita zaidi katika lile ambalo macho yangu yalilifikia kwa urahisi.Kabla ya kuanza kwa mitihani ya mwisho wa muhula niliamua kuhudhuria moja ya mikesha katika kanisa hili.Kila kitu kilikwenda sawa mpaka pale mkono uliotaka kuchomoa koromeo langu la hewa uliponinyonga.Ilikua hivi;Baada ya mkesha ule kuisha majira ya alfajiri niliamua kushika njia ili kumpumzika kabla ya kupambania maisha ya elimu yangu asubuhi iliyofuata.Katika barabara ile hakukua na watu kabisa,yawezekana wengi walikua wamelala.Haikunipa hofu sana kwani nikiwa huko paa la Afrika niliwahi kwenda mkesha mithili ya huo na haikua jambo kubwa.Leo ilikua tofauti nilikutana na watu wakitoka katika nyumba za vileo alfajiri hii na wengi hata sikuwatazama kwa marudio kwani haikunilazimu kufanya hivyo.

Nikiwa nakaribia kichochoro kilichopita dirishani kwangu na kisha kunipeleka lango la bati,nilikutana na kijana aliyeonekana kama mlevi hivi,alikua na sigara mkononi nilimpita huku nikimwazima jicho la kadri.Kabla sijarejesha jicho langu katika usawa wake,aliukamata mkono wangu na kuung’ang’ania.Kabla sijang’amua vyema nini kiliendelea walijitokeza vijana wengine wawili na hapo sasa kwa mbali nilianza kuelewa mchezo huu.Nilichukua muda kiasi kuachia simu yangu kabla ya kufikiri kuwa walikua wana wa uasi,kila kilichokuwamo ndani ya pochi ya mfukoni hakikua miliki yangu.Vyote vilivyonitambulisha kama Ashindaye vilibebwa na waasi wale,sikua na maumivu yeyote hata nilipokua chumbani kwangu.

Usingizi ulinipaa,na mapumziko yaligeuka tahajudi hata kulipokucha.Asubuhi hii maumivu yalikuwepo,maandalizi ya mitihani yalisitishwa kwani kichwa cha habari cha ‘ikomboe semista yako kwa wiki moja’kilikua kimeshafutwa na picha ya mrudiano ya uasi ule.Maumivu ya kupoteza vichache nilivyovipata kwa nguvu ya wana wa paa la Afrika yalifika hata kwenye chanzo cha umeme wa moyo.

Ubinafsi uliokithiri,kutazama mambo yetu wenyewe,uongo wa kuleta uharibifu na kujipenda zaidi hasa hata kwa kutaka vya wengine kwa nguvu yamekua maisha yaliyohalalishwa.Usiku umeendelea sana na mchana nao umekaribia,kila hazina iliyositirika ndani ya nafsi zetu itakua dhahiri kwa maisha yajayo.Kila kinachokwenda hurejea,maisha tunayowaishia wengine yana sehemu yetu katika sisi siku zijazo.

Ni wakati wa kuvivua kila viungo wa uharibifu na kurejea kwa Muumba.

Comments (5)

Leave A Comment

Enter your email address to subscribe to this blog and receive notifications of new posts by email.

Join 23,432 other subscribers

Copyright 2019 - Let's Write. All Rights Reserved

%d bloggers like this: